Na Angela Sebastian
Bukoba : Tukio la kusikitisha lililoacha simanzi limetokea katika shule ya Sekondari Bishop Kibira, iliyopo Halmashauri ya Bukoba mkoani Kagera,baada ya mwanafunzi kujinyonga.
Kamanda wa Polisi mkoani Kagera, Blasius Chatanda, amemtaja mwanafunzi huyo kuwa Jovan Revelian Justinian, mwanafunzi wa kidato cha tatu, ambaye amekutwa amefariki baada ya kujinyonga kwa shuka ndani ya moja ya bweni shuleni hapo.
Tukio hili lilitokea Juni 15, saa tisa na nusu mchana, baada ya Jovan kupatwa na msongo wa mawazo na kupotea tangu siku ya Jumapili, Juni 14 ambapo uongozi wa shule ulifanya jitihada za kumtafuta, lakini hatimaye waligundua mwili wake ukiwa umening’inia ndani ya dali la bweni, hali iliyosababisha hisia za huzuni na simanzi kwa wanafamilia, walimu, na wanafunzi.
“Uchunguzi wa awali umeonyesha kuwa, baadhi ya wanafunzi walibaki shuleni kwa sababu walikuwa wamepangwa na shule wapate masomo ya ziada kutokana na kutofikia wastani uliopangwa na shule katika mitihani yao ya nusu mwaka lakini marehemu alichukulia hali hiyo kwa hisia mbaya, na matokeo yake akachukua uamuzi wa kuondoa maisha yake"ameeleza Chatanda
Aidha, amewashauri watoto na wazazi kuwa na mazungumzo ya wazi kuhusu changamoto zinazowakumba wanapoona watoto wanapata matatizo, wasisite kuwasiliana na walimu, wazazi au wataalamu wa afya akili ili kuepusha majanga kama hayo.


