Utapeli wa Mtandaoni na Mikopo Haramu: Tishio Linalofifisha Maendeleo ya Wananchi

0

 


Na Angela Sebastian, Bukoba

“Naitwa Victor Vicent mkazi wa kijiji cha Kangabusharo, wilayani Bukoba Vijijini, kuna wakati nilikua na shida na pesa nikaingia mtandaoni nikaona kuna program ya mkopo wa mtandaoni  Inaitwa Pesa bamba wakitangaza kwa wanatoa mkopo kwa haraka bila masharti nikajiunga ili kupata huduma hiyo, Wakati najiunga walinitaka nipige picha na kuambatanisha nakala ya kitambulisho cha Taifa(NIDA) au kadi ya mpiga kura ambapo nilifanikiwa kupata mkopo wa shilingi 17,000.

Nilipaswa kurejesha mkopo huo wa ndani ya siku saba nilirejesha shiling 30,000 na kukopa tena shl.50,000 nilipatiwa 30,000 baada ya kukata riba yao, kuna siku moja kabla ya siku saba kuisha simu yangu ilizimika kwakukosa umeme, lakini baadae nilikuta wamenipigia na kunitumia jumbe za udhalilishi kupitia namba yangu nyingine ya nyumbani ambayo nawaachia watoto na kuwatumia watu wangu wa karibu akiwemo mke wangu jumbe hizo za udhalilishwaji,vitisho na matusi

Picha ya Victor Vicent mkazi wa kijiji cha Kangabusharo, wilayani Bukoba Vijijini

Hali hii inaonyesha hawa watu wanahusiana na watu wa mitandao husika na kama siyo hivyo wao wanajua vipi kama kuna ela imeingia au watu wako wa karibu ni wapi, hivyo naiomba Serikali kupitia Banki kuu ya Tanzania na mamlaka ya udhibiti wa mawasilino nchini (TCRA) kufuatilia jambo hili kwa karibu, maana wanachi wa vijijini bado wanaibiwa na kudhalilishwa sana kupitia mikopo haramu  ya mitandaoni na wezi wengine kupitia mitandao ya simu kwa sababu hawajui nani App ipi imesajiliwa.

Naiomba pia serikali kupitia benki kuu (BoT)  kuchukua hatua kali dhidi ya watu wanaoendesha huduma hizo, ikiwemo kuzifungia kabisa ili kuwalinda wananchi maana wao ndio wanaotoa usajiri huku akiomba polisi na TCRA kuweka namba maalum ya kuripoti vitendo vya udhalilishaji au vitisho vinavyotolewa na baadhi ya watoa mikopo mitandaoni. Anasimulia Victor

Simulizi hii ya Victor ni miongoni mwa visa vingi vinavyowakumba watumiaji wengi wanaotumia simu janja na data nchini Tanzania kutokana na kuomba mikopo kupitia mikopo ya mtandaoni kwa haraka bila kutathimini atahari za mikopo hiyo kutoka katika kampuni ambazo hazijasajiliwa zinazotoa huduma za kifedha kwa njia ya kidijitali.

Wakati dunia ikishuhudia ukuaji mkubwa wa huduma za kifedha za kidigitali, Tanzania nayo imekuwa miongoni mwa nchi zinazokumbwa na ongezeko la mikopo haramu na utapeli wa mtandaoni. Programu na majukwaa yasiyosajiliwa yamekuwa yakitumia ahadi za mikopo ya haraka kuwavutia wananchi lakini baadaye baadhi yao hujikuta wakipoteza fedha, kudhalilishwa na hata kuvunjika moyo katika harakati zao za kujikwamua kiuchumi.

Kutoka Bukoba hadi maeneo mengine nchini, waathirika wengi wanasema changamoto hiyo imekuwa ikiwagharimu si tu kifedha bali pia kisaikolojia. Wengi huishi kwa hofu ya vitisho, matumizi mabaya ya taarifa zao binafsi na aibu inayotokana na udhalilishaji unaofanywa na baadhi ya watoa mikopo haramu.


Matumizi ya Simu Janja na Huduma za Kifedha za Kidijitali

Kadiri matumizi ya simu janja na huduma za kifedha za kidigitali yanavyoongezeka ndivyo matapeli wanavyoendelea kubuni mbinu mpya za kuwaibia wananchi licha ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kutoa tahadhari kuhusu majukwaa ya mikopo yasiyoidhinishwa huku Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) nayo imekua ikiendelea kupokea malalamiko ya utapeli wa simu na mitandao.

Wataalamu wa usalama wa kidigitali wanaeleza kuwa, baadhi ya programu haramu za mikopo hukusanya taarifa binafsi za watumiaji zikiwemo namba za simu, orodha za mawasiliano na taarifa nyingine nyeti ambazo baadaye hutumika kuwashinikiza au kuwafedhehesha wakopaji wanaposhindwa kurejesha mikopo kwa wakati.

Mbali na kupoteza fedha, waathirika wengi hupoteza amani ya akili, kuharibiwa mahusiano na ndugu pamoja na kupoteza imani katika mifumo rasmi ya kifedha. Hali hiyo imekuwa kikwazo kwa wananchi wengi wanaotafuta njia za kuboresha maisha yao kupitia huduma za kidigitali.


Waathirika Wasilimulia Madhila ya Mikopo Haramu ya Mitandaoni

Livingstone Laulian pia ni moja ya watu walioathirika na mikopo haramu ya mtandaoni, anasema alilituma fedha akidhani kuwa atapata mkopo kupitia ujumbe alliopokea kwenye simu yangu ukieleza kuwa anaweza kupata mkopo kwa haraka baada ya kutuma fedha inayotakiwa’

Kuna zile meseji zinazotumwa kwenye namba za watu ambao unakuta hata mtu haumfahamu anakutumia ujumbe kwamba nitumie kwa Airtel Money hii jina litakuja fulani watu wanatakiwa kuwa makini sana na meseji hizo, mimi nikipata meseji kama hizi nazituma kwenda namba 15040 na kijibuwa kuwa ujumbe wangu utashughulikiwa, niliweza kuchukua hatua hizo na nisitume fedha kwasababu mimi niliisha tapeliwa na hao matapeli wa mtandaoni wakinidanganya nikituma fedha nitashughulikiwa haraka kupata mkopo na baada ya kutuma napiga simu haipatikanai tena.


Picha ya Livingstone Laulian mkazi wa Bukoba

Najiuliuza kama mamlaka za mawsiliano, benki kuu na vyombo vya ulinzi wanasema kila siku kuwa wanadhibiti sasa hii inakuwaje mtu anajua kuwa kuna fedha imeingia katika simu yako au kuna watu wanapiga kuwa kuna ela imeingia kwenye simu yako na wakati mwingine kweli umepokea muamala na pengine umeukopa kutoka katika tasisis hizo za mitandaoni,je hawa wanajuaje kama siyo wale wenye mamla husika kuna watu wasio waaminifu wanashirikiana na wezi hao

“Nilituma fedha nikiamini nitashughulikiwa haraka kupata mkopo lakini baada ya kutuma napiga simu haipatikani tena. Kuna watu wengi kule vijijini wanaendelea kuibiwa kwa njia hii kila siku,” anasema.

Hata hivyo anahoji namna matapeli hao wanavyopata taarifa za miamala ya wananchi au watu wao wa karibu.


Ujumbe wa NIDA Ulivyogeuka Mtego wa Utapeli

Meranie Rweyemamu mkazi wa Wilaya ya Bukoba anasema aliwahi kukumbana na mtandao wa utapeli uliojificha nyuma ya huduma za mikopo.

Anasema baada ya kuona tangazo la mkopo mtandaoni alituma nakala ya Kitambulisho cha Taifa kama alivyoelekezwa na kusubiri kupata huduma hiyo.

“Umeibuka wizi au utapeli mwingine kupitia mikopo hiyo ya mitandaoni mimi nimekumbana nao, niliona tangazo la mkopo kwasababu siku hiyo nilikuwa na mahitaji nikawasiliana nao maana waliweka namba yao yasimu ya mkononi nikapiga na kuambiwa nitume kitambulisho cha NIDA nikapiga picha na kutuma nikaambiwa baada ya saa 24 nitapata mkopo kwasababu bado wanakamilisha taratibu za kifedha nilivumilie.

Baada ya saa 24 kupita nikapokea ujumbe wa simu ya mkononi (SMS) iliyoandikwa hivi “NIDA. TANZANIA. Huduma zako zote za voda ZINAFUNGWA leo tar 24/05/2026 kwa kuto Rasimisha Kwa Msaada zaidi wasiliana na Mwakilishi wa NIDA”Anasema Rweyemamu.

Ameongeza kuwa baada ya kuona ujumbe huo, aliamua kuwapigia  simu kwasababu namba iliyotuma ujumbe ndio alitumia kufanya nao mawasiliano lakini jibu alilopewa ni kwamba  walipoangalia kwenye mfumo wamekuta line yake inapaswa kufungwa kwasababu  hajalasimisha NIDA hivyo anapaswa atume shilingi 50,000 ili wamuunganieshe na ofis za NIDA na  kulasimishwa ili apate mkopo.

“Nilipokuwa natafuta taarifa zaidi mtandaoni niliona elimu ya NIDA ikisema wananchi wafike ofisini wanapokuwa na changamoto. Nilipoenda NIDA niliambiwa wale ni matapeli,

Anasema baada ya kurejea nyumbani na kujaribu kuwapigia simu tena, simu hizo hazikupatikana jambo lililomthibitishia kuwa alikuwa akilengwa na mtandao wa utapeli.’ Amesema


NIDA Yawataka Wananchi Kuupuza Ujumbe wa Matapeli Kupitia Simu za Mkononi

Kufuatia matukio ya wananchi kutumiwa ujumbe kupitia simu zao za mkononi, Afisa Habari wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) Makao Makuu, Alphani Mlacha anawashauri wananchi kupuuza jumbe hizo zinazotumwa na watu wanaojifanya watumishi wa NIDA.

Mlacha anasema kuna matapeli wanaotumia jina la NIDA kuwalaghai wananchi kwa kutuma ujumbe wa simu na kuwataka kutuma fedha au taarifa binafsi.

Picha ya Afisa Habari wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) Makao Makuu, Alphani Mlacha akitoa ushauri wananchi kupuuza jumbe hizo zinazotumwa na watu wanaojifanya watumishi wa NIDA.

“Ukiona watu wanadukua kitu fulani au huduma fulani ujue huduma hiyo ni ya muhimu sana kwa jamii. NIDA ni taasisi muhimu kwa wananchi hivyo wasidanganyike na watu wenye nia ovu. Mtu yeyote mwenye changamoto kuhusu NIDA afike ofisini au awasiliane na kituo chetu cha huduma kwa wateja kupitia namba 0232210500,” Amesema Mlacha.


BoT Yatoa Onyo Kali kwa Waendesha Programu za Mikopo Haramu ya Mtandaoni

Meneja Msaidizi wa Idara ya Mawasiliano wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Noves Moses anasema baadhi ya programu za mikopo zisizosajiliwa zimekuwa zikitumia mbinu za udhalilishaji kwa wakopaji.

Anasema baadhi ya watoa mikopo hao huchukua taarifa za wakopaji kisha kuwasiliana na ndugu au marafiki zao kwa lengo la kuwashinikiza kulipa madeni huku wakitumia lugha za vitisho, matusi na udhalilishaji.

“BoT kwa kushirikiana na mamlaka nyingine za kisheria inaendelea kuzifuatilia programu hizo ili kuzifungia na kuwachukulia hatua wahusika

Picha ya Meneja Msaidizi wa Idara ya Mawasiliano wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Noves Moses anakitoa elimu kuhusu mikopo ya mtandaoni

Tunaendelea kupokea taarifa kutoka kwa wananchi kuhusu programu zisizosajiliwa. Tunazifuatilia na kuzibaini na pale inapothibitika zinakiuka sheria tunazifungia,”Amesema Moses.


Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) Yawataka Wananchi Kuchukua Tahadhari


Meneja wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania(TCRA), Kanda ya Ziwa, Mhandisi Imelda Banali anasema uhalifu wa mtandaoni ni sawa na uhalifu mwingine wowote na unasimamiwa na Sheria ya Makosa ya Mtandao ya mwaka 2015.

Amesema uhalifu wa aina yoyote uwe wa mtandaoni au wa ana kwa ana wote ni uhalifu hivyo hata sheria inayotumika katika makosa ya uhalifu mtandaoni Cybercrimes Act.


Picha ya Meneja wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania(TCRA), Kanda ya Ziwa, Mhandisi Imelda Banali akieleza kuhusu Sheria ya Makosa ya Mtandao ya mwaka 2015

Sura ya 114A ya Sheria ya Tanzania, ya mwaka 2015 ambayo husimamiwa na jeshi la polisi ambapo nafasi ya TCRA ni kuhakikisha tunaweka utaratibu wa watu kupata taarifa na kuelewa kuwa akitumiwa ujumbe au kupewa maelekezo kupitia mtandaoni ajilidhishe kwanza

“Wananchi wanapaswa kujiridhisha kabla ya kutuma fedha au kutoa taarifa binafsi kwa watu wasiowafahamu.

Mfano zinazohusu tuma pesa kwanza, mikopo, nafasi za kazi au mtoto wako ameugua, mwananchi anatakiwa kujiridhisha kwanza kabla ya kuchukua hatua. Ndiyo maana tumeweka namba maalum ya kutoa taarifa ambayo ni 15040,”Amesema Banali.


Polisi Wahimiza Wananchi Kuripoti Matukio ya Utapeli


Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kagera, Blasius Chatanda anawashauri wananchi kuchukua tahadhari wanapokutana na ujumbe wa kutuma fedha au kujiunga na programu za mikopo ambazo hawana uhakika nazo.

Anasema ni muhimu kutoa taarifa polisi na kwa taasisi husika mara wanapokumbana na vitendo vya utapeli wa mtandaoni.


Picha ya Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kagera, Blasius Chatanda akitoa ushauri kwa wananchi kuchukua tahadhari wanapokutana na ujumbe wa kutuma fedha au kujiunga na programu za mikopo

Sheria ya Makosa ya Mtandao ya mwaka 2015 imeweka masharti ya kudhibiti uhalifu unaofanyika kupitia mifumo ya kidigitali ikiwemo ulaghai wa kifedha na matumizi mabaya ya mifumo ya mawasiliano.

Kwa mujibu wa vifungu vya 16 na 17 vya sheria hiyo, mtu anayefanya ulaghai wa kifedha kwa njia ya mtandao anaweza kuadhibiwa kwa kifungo cha jela pamoja na faini.


Je Serikali Inafanya nini Kukabiliana na Utapeli kwa Njia ya Mtandao


Serikali imeendelea kuhamasisha wananchi kuhusu hatari za mikopo haramu na utapeli wa mtandaoni huku ikiimarisha mifumo ya usalama wa kidigitali na usimamizi wa huduma za kifedha.

Pia mamlaka mbalimbali zimeendelea kushirikiana katika kubaini na kuchukua hatua dhidi ya majukwaa yasiyosajiliwa pamoja na wahalifu wanaotumia teknolojia kuwaibia wananchi.

Hadithi za Victor, Livingstone na Meranie zinaonyesha kuwa mikopo haramu ya mitandaoni si tatizo la kifedha pekee bali pia ni janga la kijamii na kisaikolojia linalowaathiri wananchi wengi. Wakati wengine wakipoteza fedha, wengine hujikuta wakikabiliwa na fedheha, vitisho na matumizi mabaya ya taarifa zao binafsi.

Tafiti zinaonyesha kuwa  inavyoendelea kupanua matumizi ya huduma za kidigitali, ndivyo umuhimu wa elimu ya usalama mtandaoni unavyozidi kuongezeka. Wataalamu wanaeleza kuwa wananchi wanapaswa kujiridhisha kuhusu uhalali wa huduma wanazotumia, kuepuka kutuma fedha kwa watu wasiowafahamu na kuripoti mara moja matukio ya utapeli kwa mamlaka husika.

Bila tahadhari na ushirikiano wa pamoja, mikopo haramu ya mitandaoni itaendelea kufifisha ndoto, mipango na malengo ya maendeleo ya wananchi wengi wa Tanzania.






Chapisha Maoni

0 Maoni
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.
Chapisha Maoni (0)

#buttons=(Accept !) #days=(20)

Our website uses cookies to enhance your experience. Learn More
Accept !
To Top