Serikali kupitia Wizara ya Kilimo imeanza kusambaza Mwongozo wa Matumizi ya Ghala za Umma, hatua inayolenga kuongeza ufanisi wa matumizi ya maghala na kuimarisha usalama wa chakula nchini.
Zoezi hilo linafanywa na timu ya wataalam kutoka Wizara ya Kilimo mkoani Kigoma kwa lengo la kuhakikisha maghala ya Umma na yale yanayomilikiwa na Sekta Binafsi yanatumika kwa tija na kwa kuzingatia taratibu rasmi.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa kikao kazi cha kusambaza mwongozo huo tarehe 11 Mei 2026, Katibu Tawala Msaidizi anayeshughulikia Uchumi na Uzalishaji mkoani Kigoma, Bw. James Peter amesema kuwa mwongozo huo ni hatua muhimu katika kuhakikisha maghala yote yanatumika kwa malengo yaliyokusudiwa.
“Naishukuru Serikali kwa kufanikisha utoaji na usambazaji wa mwongozo huu. Sote ni mashuhuda wa uwepo wa maghala yaliyojengwa na Serikali, yanayomilikiwa na Serikali pamoja na yale ya watu binafsi. Tukiyaangalia kwa pamoja, tunaweza kuona ni yapi yanafanya kazi ipasavyo na yapi hayatumiki kikamilifu,” amesema Bw. James Peter.
Ameeleza kwa muda mrefu wadau wa kilimo wamekuwa wakitamani kuona maghala yanatumika ipasavyo ili kupunguza changamoto za upotevu wa mazao baada ya kuvuna, hali inayochangia kuimarisha usalama wa chakula.
✍️wizara ya kilimo


