Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo, Bw. Gerald Mweli, amesema Serikali ya Tanzania inaendelea kuthamini mchango wa washirika wa maendeleo katika kuimarisha sekta ya kilimo, hususan kupitia uwekezaji katika mifumo himilivu na mabadiliko ya tabianchi katika kumuinua mkulima mdogo.
Mweli amesema hayo wakati wa hafla ya utiaji saini wa Hati ya Makubaliano (MoU) kati ya International Fund for Agricultural Development (IFAD) na Agence Française de Développement (AFD) kwa ajili ya utekelezaji wa Mradi wa Kuboresha Sekta ya Maziwa kwa njia himilivu dhidi ya mabadiliko ya tabianchi (Climate-Smart Smallholder Dairy Transformation Project – C-SDTP). Hafla hiyo ilifanyika pembezoni mwa mkutano uliofanyika Jijini Nairobi, Kenya, kuanzia tarehe 11 hadi 12 Mei 2026, ambapo Mheshimiwa Waziri Mkuu anamwakilisha Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Mweli amesema ushirikiano huo unaonesha imani kubwa ya washirika wa maendeleo katika ajenda ya Tanzania ya mageuzi ya kilimo na juhudi za kujenga mifumo ya chakula iliyo imara, endelevu, na himilivu dhidi ya mabadiliko ya tabianchi.
Hafla hiyo imehudhuriwa na Balozi wa Tanzania nchini Ufaransa, Mhe. Said Othman Yakubu; Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara, Bw. Aristides Robert Mbwasi; Kamishna wa Fedha za Nje kutoka Wizara ya Fedha, Bw. Rashed Bade; wataalam kutoka Wizara ya Kilimo; pamoja na wadau wa maendeleo kutoka IFAD na AFD
✍️wizara ya kilimo


