Kamati ya Shindano la Vijana Uchumi Challenge ikiongozwa na Mwenyekiti wake Bw. Joseph Brighton Malekela, imeongeza muda wa mwisho wa kushiriki shindano hilo kutoka tarehe 30 Aprili, 2026 mpaka Mei 7, 2026.
Amesema kuwa uamuzi huo umetokana na ushauri uliotolewa na vijana, Maafisa Vijana pamoja na wadau wa maendeleo ya vijana, kutoka Halmashauri na Mikoa mbalimbali wanaotaka kuona shindano hilo linabeba sura ya kitaifa kwa kuongeza ushiriki wa vijana kutoka maeneo mbalimbali nchini.
“Ombi hili limeonyesha hamasa kubwa, uhitaji wa ushiriki mpana zaidi na mwitikio chanya kutoka kwa vijana na wadau wanaotamani kuona shindano hili linakuwa na manufaa zaidi kwa vijana wanaoshiriki.
Ameeleza kuwa, kwa takwimu za awali mkoa wa Dar es salaam unaongoza kwa ushiriki kwa kuwa na 27.62%, ukifuatiwa na Mjini Magharibi (Zanzibar) kwa 10.67%, Dodoma (5.88%), Morogoro (4.99%) na Mwanza (4.88%).
Aidha, amebainisha kuwa mikoa yenye ushiriki mdogo ni pamoja na Rukwa (0.90%), Songwe (0.79%) na Katavi (0.54%).
Ameongeza kuwa Mawazo yanayotakiwa kuwasilishwa yanapaswa kuwa na sifa saba ambazo ni ubunifu, uelewa wa changamoto za kiuchumi, uhalisia, kukuza uchumi wa taifa, uwezo wa Kuleta fursa, uendelevu na ubora wa uwasilishaji.
Shidano la “Vijana Uchumi challenge” lilitambulishwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Maendeleo ya Vijana Mhe. Joel Arthur Nanauka, tarehe 10 Aprili, 2026 kwa lengo la kukuza uchumi na kuwezesha taifa kujitegemea hasa wakati wa kipindi cha athari za misukosuko ya kimataifa.


