Na Ghati Msamba-Mara
Taasisi ya Community Alive inayojihusisha na utoaji wa huduma kwa watoto wanaoishi katika mazingira magumu, imetoa mafunzo kwa wadau mbalimbali kuhusu namna ya kupambana na ukatili dhidi ya watoto.
Mafunzo hayo yalifanyika Mei 16, 2026 katika ukumbi wa Pachel uliopo Kanisa Katoliki Musoma mjini, yakihusisha wadau wa ustawi wa jamii, elimu pamoja na jamii kwa ujumla.
Mwezeshaji wa semina hiyo ambaye ni Afisa Ustawi wa Jamii wa Halmashauri ya Manispaa ya Musoma, Freddy Edward, alisema watoto wana haki mbalimbali za msingi ikiwemo haki ya kushiriki na kutoa maoni yao, kusikilizwa, kupewa majina na wazazi wao pamoja na kupata haki ya utaifa kupitia cheti cha kuzaliwa.
Edward alieleza kuwa kwa mujibu wa Sheria ya Mtoto ya mwaka 2009, mtoto anatakiwa kulindwa na kusimamiwa tangu akiwa tumboni hadi anapofikisha umri wa miaka 18. Alisema sheria hiyo ilifanyiwa maboresho mwaka 2019 kutokana na kuongezeka kwa changamoto za ukatili, unyanyasaji na ukiukwaji wa haki za watoto katika jamii. Aidha, alisisitiza kuwa malezi bora, ushirikiano wa familia, jamii na taasisi mbalimbali ni msingi muhimu katika kuhakikisha watoto wanakua katika mazingira salama na yenye kuzingatia haki zao za msingi.
Kwa upande wao, wadau walioshiriki mafunzo hayo walisema elimu inapaswa kutolewa zaidi kwa wanafunzi mashuleni ili mtoto anapofanyiwa ukatili aweze kutoa taarifa kwa mwalimu au mamlaka husika kwa wakati. Pia walisisitiza kuwa kila mzazi na mlezi ana wajibu wa kumtunza, kumlinda na kuhakikisha mtoto anapata haki zake zote za msingi. Vilevile, walizitaka taasisi za kiraia pamoja na serikali kuendelea kufanya makongamano na kampeni za mara kwa mara kwa jamii ili kuongeza uelewa kuhusu madhara ya ukatili dhidi ya watoto.
Wadau hao walibainisha kuwa baadhi ya sababu zinazosababisha ukatili dhidi ya watoto ni pamoja na ugumu wa maisha na hali duni ya uchumi, migogoro ya kifamilia na ugomvi wa wazazi mbele za watoto, mila na desturi za baadhi ya makabila, wazazi kutofahamu haki za watoto, matumizi mabaya ya mitandao ya kijamii, uzazi usio na mpangilio, ongezeko la watoto wa mitaani pamoja na migogoro inayotokana na ndoa za wake wengi.
Aidha, walisema ili kupunguza na hatimaye kutokomeza vitendo vya ukatili dhidi ya watoto, jamii inapaswa kuhakikisha watoto wanapatiwa haki zao za msingi, kupewa elimu bora, kushirikishwa katika masuala yanayowahusu pamoja na kulelewa katika mazingira salama yenye upendo na malezi bora.
Kwa upande wake, Mratibu wa Miradi wa Taasisi hiyo, Daniel Msangya, alisema mradi huo ulianzishwa mwaka 1995 ukiwa na lengo la kuboresha maisha ya watoto wanaoishi katika mazingira magumu kwa kuwapatia elimu ya msingi na sekondari, huduma za afya pamoja na mafunzo ya ujuzi na stadi za kazi ili waweze kutimiza ndoto zao.
Msangya alisema kwa sasa watoto wapatao 40 wapo ndani ya mradi huo huku zaidi ya watoto 300 wakipata huduma mbalimbali. Aliongeza kuwa watoto wenye umri kuanzia mwaka mmoja hupatiwa huduma za afya, huku wenye umri wa miaka 5 hadi 18 wakipata elimu, huduma za afya pamoja na mafunzo ya ujuzi wa kazi. Alisema hadi sasa zaidi ya watoto 2,000 wamefanikiwa kupitia huduma zinazotolewa na taasisi hiyo.
Hata hivyo, ametaja changamoto kubwa kuwa ni ukosefu wa ufadhili wa kutosha wa kifedha, akisema endapo watapata wafadhili zaidi wataweza kuongeza wigo wa huduma na kufikia idadi kubwa zaidi ya watoto wanaoishi katika mazingira magumu.





