Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo anayesimamia Maendeleo ya Mazao na Usalama wa Chakula, Prof. Peter L. M. Msoffe, ameitaka Menejiment ya Kampuni ya Mbolea Tanzania (TFC) kuongeza kiwango cha upatikanaji wa mbolea nchini ili kumwezesha mkulima kufanya shughuli za kilimo wakati wote wa msimu.
Prof. Msoffe ameeleza hayo tarehe 20 Aprili 2026, jijini Dad es Salaam na kuongeza kuwa usalama wa chakula ni suala muhimu kwa nchi yetu, hivyo TFC ina jukumu la kuhakikisha mbolea inapatikana kwa wakulima wakati wote wa uzalishaji wa mazao.
Pia ameeleza kuwa kutokana na Serikali kusisitiza uhifadhi na utunzaji wa mazingira ni wakati sasa TFC kuingia ubia na Halmashauri ili kuzalisha mbolea zisizo za kemikali zinazotokana na taka za majumbani.
Aidha, amesisitiza TFC kujiendesha kibiashara kwa kutafuta wawekezaji walio tayari kuwekeza nchini ili kuongeza kiwango cha uzalishaji wa mbolea ndani ya nchi sambamba na kukuza biashara ya mbolea.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya Mbolea Tanzania (TFC), Bw. Samuel Mshote ameeleza kuwa pamoja na changamoto zinazoendelea katika nchi za Ghuba, TFC itahakikisha mbolea inapatikana kwa wakulima na kwa wakati.
✍️wizara ya kilimo


