Serikali Kuanzisha Madawati ya Polisi Kudhibiti Rushwa Katika Vyama vya Ushirika

0


Waziri wa Kilimo, Mhe. Daniel Chongolo (Mb), amesema Serikali iko katika hatua za kupanga kushirikiana na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) pamoja na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi ili kuanzisha madawati maalum ya kipolisi yatakayoshughulikia masuala ya vyama vya ushirika nchini.

Akizungumza jijini Dodoma tarehe 24 Aprili 2026 wakati wa uzinduzi wa kampeni ya “Linda Ushirika, Chagua Uadilifu”, Mhe. Chongolo amesema kuwa lengo la mpango huo ni kuimarisha uwajibikaji, kudhibiti vitendo vya rushwa na ubadhirifu, pamoja na kuhakikisha wahusika wanachukuliwa hatua za kisheria bila upendeleo.

Amesisitiza kuwa Serikali haitavumilia vitendo vya viongozi wa vyama vya ushirika wanaotumia vibaya rasilimali za wanachama, akitoa mfano wa AMCOS ya Sikonge iliyopoteza zaidi ya Shilingi Bilioni 1.2 kutokana na ubadhirifu. Aidha, amekemea vitendo vya udanganyifu katika ununuzi wa mazao, ikiwemo uchezeaji wa mizani.

Mhe. Chongolo amebainisha kuwa ushirika unachangia zaidi ya Shilingi Trilioni 6, hivyo inahitaji mifumo madhubuti ya usimamizi ili kulinda maslahi ya wanachama na kukuza uchumi wa wakulima.

Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhe. Ayoub Mohamed Mahmoud (Mb), ameeleza utayari wa Wizara yake kushirikiana katika kuimarisha usalama na kudhibiti vitendo vya uhalifu ndani ya vyama vya ushirika.

Naye Mwakilishi wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Viwanda, Biashara na Uvuvi, Mhe. Ghati Chomeke (Mb), amesisitiza umuhimu wa kuongeza elimu kwa wanaushirika kuhusu masoko na thamani ya mazao ili kuboresha maamuzi ya kibiashara na kuongeza kipato.

✍️wizara ya kilimo

Chapisha Maoni

0 Maoni
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.
Chapisha Maoni (0)

#buttons=(Accept !) #days=(20)

Our website uses cookies to enhance your experience. Learn More
Accept !
To Top