Na SETH KAZIMOTO, Mahakama-Arusha
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Arusha, Mhe. Frank Mahimbali amesema kuwa, Mahakama ni mali ya wananchi na kwamba Mahakama hizo zipo kwa ajili kuwahudumia wananchi.
Mhe. Mahimbali ambaye alikuwa Mgeni Rasmi wakati wa hafla ya uzinduzi wa Mahakama za Mwanzo mpya tatu za Ketembeine, Makuyuni na Terrat zilizopo mkoani Arusha uliofanyika tarehe 10 Aprili 2026 katika Mahakama ya Mwanzo Makuyuni wilayani Monduli.
Jaji Mfawidhi huyo alisisitiza kuwa, tukio hilo la uzinduzi na urasimishaji wa Mahakama hizo ni hatua muhimu katika kuimarisha upatikanaji wa haki kwa wananchi wote wa Tanzania na ujenzi wa Mahakama hizo ni matunda ya dhamira ya Serikali ya kuhakikisha kuwa, wananchi wote wanapata haki mapema ipasavyo na kwa gharama nafuu.
“Kwa muda mrefu, wananchi wa maeneo hayo wamekuwa wakisafiri umbali mrefu kufuata huduma za Mahakama, kwa mfano; wananchi wa Kata za Makuyuni, Mswakini, Esiraeli na Nanja walikuwa wakisafiri umbali wa kilomita 36 kwenda katika Mahakama ya Mwanzo Mto wa Mbu au kusafiri kilomita takribani 70 kwenda katika Mahakama ya Mwanzo Kisongo iliyopo Monduli mjini ili kupata huduma, hivyo ujenzi wa Mahakama hizi umesogeza huduma kwa wananchi hao,” alisema Jaji Mahimbali.
Vilevile Mhe. Mahimbali aliongeza kuwa, kusafiri umbali mrefu kufuata huduma za Mahakama kulisababisha baadhi ya wananchi kukata tamaa na kuacha kufuatilia mashauri yao na hivyo kupoteza haki zao. Pia wananchi wengine walikuwa wakiamua kujichukulia sheria mkononi mwao, hivyo Mahakama hizo zinazozinduliwa zinakwenda kuhudumia jamii zinazozizunguka Mahakama hizo kwa kusogeza huduma karibu na makazi yao na hivyo kurahisisha upatikanaji wa haki na kupunguza muda wa kupata haki, hivyo kutumia muda wao mwingi katika shughuli za kiuchumi na kujiongezea kipato.
✍️mahakama Tanzania











