Mwandishi Wetu, Serengeti.
Wanawake wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Mkoa wa Mara wametembelea kituo cha Hope Mugumu kilichopo Wilaya ya Serengeti kinachotoa hifadhi kwa mabinti waliokimbia aina mbalimbali za ukatili wa kijinsia ukiwemo ukeketaji na ndoa za utotoni, na kukabidhi msaada wa mahitaji mbalimbali.
Wanawake hao wamekabidhi mahitaji hayo Machi 8, 2026 ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya siku ya wanawake duniani. Ambapo wamekabidhi mahitaji ikiwa ni pamoja na madaftari, unga wa ngano, sukari, unga wa mahindi, taulo za kike, sabuni, dawa za meno, miswaki na vinywaji (soda).
Akizungumza kwa niaba ya wanawake hao Tecla Chipeta amesema kuwa huo ni utaratibu waliojiwekea wa kusaidia wahitaji ili kuwaletea furaha na tabasamu, kama sehemu ya kuonesha upendo kwa jamii.
Aidha, Chipeta amemshukuru Rhobi Samwelly, Mkurugenzi wa Shirika la Hope for Girls and Women in Tanzania, linalomiliki kituo hicho, kwa moyo wake wa upendo kwa kuanzisha kituo kinachotoa hifadhi kwa wasichana waliokimbia ukeketaji na ndoa za utotoni kutoka katika familia zao.
Amepongeza kwa kusema kuwa, mbali na kuwapa hifadhi, wasichana hao pia wanaendelea na masomo wakiwa kituoni hapo ili waweze kutimiza ndoto zao jambo ambalo ni jema katika maisha yao kwa siku za usoni.
Pia, Chipeta amewataka mabinti waliopo kituoni hapo kusoma kwa bidii, kumtanguliza Mungu katika maisha yao na kutambua kuwa hawapo peke yao.
Pia, amewaomba wadau mbalimbali kujitokeza na kuendelea kuunga mkono jitihada hizo kwa kutoa misaada ya mahitaji mbalimbali, badala ya kumwachia jukumu hilo Mkurugenzi wa shirika hilo pekee.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Shirika hilo Rhobi Samwelly, amewashukuru wanawake hao wa TRA kwa moyo wao wa upendo na kujitoa, akisema msaada huo utasaidia kwa kiasi kikubwa mahitaji ya wasichana waliopo katika kituo hicho.
“Tumefarijika sana kwa msaada wenu ambao Mungu amewagusa kuleta hapa. Mungu azidishe baraka nyingi kwa kile mlichotoa na awarudishie mara dufu. Wasichana hawa wamefurahishwa na ujio wenu na mmewatia moyo kusoma kwa bidii. Mwambieni Meneja wa TRA Mkoa wa Mara pamoja na watumishi wote wa TRA kuwa tumefurahi sana kwa upendo wenu,” amesema Rhobi.
Aidha, Rhobi amesema kuwa Shirika la Hope for Girls and Women in Tanzania, lina vituo viwili vinavyotoa hifadhi kwa wasichana waliokimbia ukatili wa aina mbalimbali. Kituo cha Hope Mugumu kina jumla ya wasichana 92, huku kituo Cha Butiama Nyumba Salama kilichopo Kiabakari kikiwa na mabinti 87, wanaopatiwa hifadhi na huduma mbalimbali.





