Vijana Kada za Afya Waja na Mpango wa Elimu Rafiki

0


Na Mwandishi wetu, WAF- Dodoma 

Wanafunzi wa fani za afya kutoka mikoa ya Mwanza, Dodoma, na Dar es Salaam wamezindua mpango maalum wa kutoa elimu kwa vijana wa shule za msingi, sekondari, na makundi maalum, lengo ikiwa ni kujenga jamii yenye afya bora kimwili na kiakili.

Akizungumza katika kikao cha kitaalam jijini Dodoma, kilichowakutanisha wataalam kutoka wizara husika na TAMIDA Initiative, Mwenyekiti Msaidizi wa taasisi hiyo, Godson Madeha, amesema lipo pengo kubwa la elimu sahihi kwa vijana, hasa katika masuala ya afya ya akili, uzazi, na lishe. 

"Kupitia mpango huu tunataka kuhakikisha vijana wanapata taarifa sahihi, kwa wakati unaofaa na kwa njia rafiki, ili waweze kufanya maamuzi bora kuhusu maisha yao.” amesema Madeha.

Madeha amebainisha kuwa kupitia ushirikiano na Serikali, vijana wengi zaidi watafikiwa kwa njia rafiki, jambo litakalosaidia kupunguza changamoto za afya ya akili na kuongeza uelewa sahihi wa masuala ya afya ya uzazi.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa TAMIDA Initiative, Loveness Kimaro, amesema kuwa taasisi hiyo imejipanga kuhakikisha elimu inayotolewa inajenga uwezo wa kijana kufanya maamuzi sahihi kuhusu afya na maisha yao kwa ujumla.

“Tunataka kujenga kizazi chenye uelewa na uwezo wa kujisimamia. Vijana wakipata elimu sahihi mapema, wanakuwa na msingi imara wa kukabiliana na changamoto za kiafya na kijamii,” amesema Kimaro.

Kimaro ameongeza kuwa kuhusisha vijana moja kwa moja katika mchakato wa kujifunza huongeza uelewa, kujiamini, na uwezo wa kukabiliana na changamoto mbalimbali, ikiwemo msongo wa mawazo na lishe duni.

Akiongea wakati wa hafla hiyo Mtaalam wa Lishe kutoka TAMIDA Initiative, Husna Boniphace, amesisitiza umuhimu wa lishe bora kwa ukuaji na maendeleo ya vijana, huku akibainisha kuwa ukosefu wa elimu sahihi ya lishe umesababisha changamoto nyingi za kiafya.

“Lishe bora ni msingi wa afya njema, Vijana wanahitaji kuelewa wanachokula, kwa kiasi gani, na kwa nini, ili waweze kujenga miili yenye afya, nguvu ya kujifunza, na kufanya kazi,” amesema Boniphace.

Mpango huu unatoa njia mpya ya kushirikisha vijana moja kwa moja, kuondoa pengo la elimu ya afya, na kukuza kizazi chenye uwezo wa kufanya maamuzi sahihi. 

Mpango huu unatekelezwa kwa kushirikiana na Serikali kupitia Wizara ya Afya, Wizara ya Elimu, na Ofisi ya Waziri Mkuu – TAMISEMI, chini ya uratibu wa taasisi isiyo ya kiserikali ya TAMIDA Initiative, iliyozinduliwa mwaka 2024. Mpango unalenga kuwafikia vijana kwa taarifa sahihi, rafiki, na zinazokidhi mahitaji yao halisi.

✍️wizara ya afya







Chapisha Maoni

0 Maoni
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.
Chapisha Maoni (0)

#buttons=(Accept !) #days=(20)

Our website uses cookies to enhance your experience. Learn More
Accept !
To Top