Waziri wa Kilimo, Mhe. Daniel Chongolo (Mb) ameeleza kuwa Tanzania na Italia zimekuwa zikishirikiana kwa miaka mingi katika masuala ya maendeleo ikiwemo Sekta ya Kilimo, ambapo miaka ya 1990 Tanzania ilipokumbwa na janga la ukame nchi ya Italia ilitoa msaada wa chakula kwa Serikali ya Tanzania.
Ameeleza hayo alipokutana kwa mazungumzo na Balozi wa Italia nchini Tanzania, Mhe. Giuseppe S. Coppola tarehe 17 Machi 2026 jijini Dar es Salaam.
“Tanzania imekuwa na ushirikiano mkubwa na Italia kupitia programu inayoitwa Mattei Plan Initiative. Katika programu hiyo Tanzania tunatarajia kunufaika na mradi wa uhimilivu wa chakula, uongezaji wa thamani katika zao la Kahawa na ufadhili wa kuiwezesha Benki ya Maendeleo ya Kilimo,” amesema Mhe. Chongolo.
Ameongeza kuwa kuiwezesha Benki ya Wakulima ni sawa na kuwawezesha wakulima nchini ambapo watapata mtaji kwa lengo la kuongeza uzalishaji na kulima kwa kisasa.
Kwa upande wake, Mhe. Balozi Coppola ameeleza kuwa Serikali yake ina dhamira ya kukuza ushirikiano kwa kuwekeza katika Sekta ya Kilimo hususan kwenye teknolojia ya kuongeza thamani katika zao la Kahawa; ikiwa ni pamoja na kubadilishana uzoefu.
✍️wizara ya kilimo


