Suala la kutokomeza vitendo vya ukatili wa kijinsia linahitaji ushirikiano -Dkt. Homera

0



Na MARY GWERA, Mahakama-Dodoma

Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Dkt. Juma Zuberi Homera (MB) amesema kuwa, Ukatili wa Kijinsia (GBV) si tu ukiukaji wa kisheria bali ni jeraha la kijamii linalokua kwa ukimya, hofu, pamoja na mila na desturi hatarishi kama vile ukeketaji hivyo ni jukumu la Majaji, Mahakimu wanawake na kila mmoja katika jamii kutokomeza vitendo hivyo na kuhakikisha haki inapatikana.

Akizungumza   tarehe 10 Machi, 2026 wakati akifungua Kongamano Maalum la Kusherehekea Siku ya Kimataifa ya Majaji na Mahakimu Wanawake katika ukumbi wa ‘New Generation’ jijini Dodoma, Mhe. Dkt. Homera amesema kuwa Majaji na Mahakimu Wanawake si tu watekelezaji wa sheria, bali pia ni walinzi wa amani ya jamii na watetezi wa haki za binadamu.

Waziri huyo amesema, wakati waathirika wanapofika Mahakamani, wanabeba maumivu, aibu na mara nyingine kutokuwa na imani na wale wanaowazunguka, hivyo ameeleza, “ninyi kama Majaji wanawake, uwepo wenu katika tasnia ya utoaji haki unatoa unatia faraja na kuleta tumaini la upatikanaji wa haki wanawake wengine walio tendewa vibaya. ”

Kwa upande wa Tanzania, Kaulimbiu ya maadhimisho hayo inasema, “Kutoka katika kuta za Mahakama hadi katika Jamii: Majaji Wanawake Wakiongoza Mapambano Dhidi ya Ukatili wa Kijinsia,” Mhe. Dkt. Homera amesema kauli mbiu hiyo inaendana na kaulimbiu ya kimataifa inayosema: “Majaji Wanawake Ndani na Nje ya Mahakama: Wakilinda Upatikanaji wa Haki,”  

Waziri huyo amekipongeza Chama cha Majaji na Mahakimu Wanawake Tanzania (TAWJA) kwa kuipa uzito Siku ya Kimataifa ya Majaji Wanawake tangu mwaka 2023 baada ya Azimio la Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa lililopitishwa tarehe 26 Aprili 2021 huko Doha nchini Qatar.

Katika hatua nyingine, Mhe. Dkt. Homera ameupongeza uongozi wa Mahakama ya Tanzania kwa hatua kubwa ya mafanikio iliyopiga katika uboreshaji wa huduma za utoaji haki nchini.

‘Hapa napenda kutoa pongezi kwa Mahakama ya Tanzania chini ya uongozi wa Mheshimiwa George M. Masaju, Jaji Mkuu wa Tanzania, kwa mabadiliko makubwa yaliyoimarisha upatikanaji wa haki,’ amesema Waziri huyo.

Ameongeza kuwa, katika muda wangu mfupi tangu aanze majukumu yake Wizara Katiba na Sheria amevutiwa na maendeleo ya Mahakama katika suala zima la matumizi ya teknolojia katika utoaji wa haki ambapo amesema Mahakama imejizatiti kwa ajenda ya kisasa na mpango wa usikilizaji mashauri kwa njia ya Mahakama mtandao, ikitoka katika matumizi ya karatasi na kuelekea mfumo wa kidijitali.

Ametaja miongoni mwa mabadiliko yenye athari chanya kuwa ni pamoja na Mfumo wa kielektroniki wa kusajili na kuendesha Mashauri (JoT-eCMS) ambao umesaidia kuondoa ucheleweshaji wa usikilizwaji wa mashauri, kuongeza uwazi na kuimarisha usimamizi wa mashauri ya familia na ukatili wa kijinsia.

Waziri huyo amesema mabadiliko mengine ni uwepo wa Vituo Jumuishi vya Utoaji Haki (IJCs), ambapo ameeleza hadi sasa kuna vituo jumuishi zaidi ya tisa nchi nzima vilivyokwisha jengwa na vinavyoendelea kujengwa.

Ameongeza kwamba, Kituo Jumuishi cha Masuala ya Familia  kilichopo Temeke mkoani Dar es Salaam kimetoa mafanikio makubwa ikiwa ni ushahidi wa maono ya Serikali kwa kushirikiana na Mahakama. Kwa mwaka 2025, Mahakama hiyo ilishughulikia mashauri zaidi ya 9,200, yakiwemo ya ukatili wa kijinsia na familia, lakini pia iliwezesha asilimia 61 ya wanawake kupata msaada wa kisheria jambo linaloonyesha wazi kuwa, zinapounganishwa huduma za Mahakama, Polisi, na Ustawi wa Jamii katika eneo moja, vizuizi vya upatikanaji wa haki kwa wanawake vinaanza kupungua.

Kadhalika, Mhe. Dkt. Homera ameongeza mafanikio mengine ya Mahakam ani pamoja na kuwepo kwa Uwajibikaji Unaotegemea Takwimu kupitia mfumo wa kanzi data (Data Hub), Mahakama inaonesha jinsi inavyoshughulikia mashauri nyeti ya ukatili wa kijinsia (GBV) kwa wakati halisi na kuhakikisha mashauri hayo muhimu yanatatuliwa haraka.

Hata hivyo, Waziri huyo ametoa rai kwa Mahakama kuwa, panapo mafanikio hapakosi changamoto hivyo ni lazima iwe makini na changamoto zilizopo.

“Mnapaswa kushughulikia ubaguzi wa kidijitali, mnatakiwa kuipeleka haki hii hasa ya matumizi ya teknolojia katika hatua nyingine kwa kuhakikisha huduma hii si kwa watu wa mijini tu bali pamoja na watu walio pembezoni, vilevile ni muhimu kuhifadhi kumbukumbu nyeti za Mahakama kwa viwango vya juu vya ulinzi wa kanzi data ili kuepuka kuvujisha siri za waathirika,” ameeleza.

Ameihakikishia Mahakama kuwa, Wizara itaendelea kushirikiana kwa karibu na Mhimili huo kuhakikisha mifumo ya kisheria inaendana na ulinzi wa athari za teknolojia.

Kadhalika, Waziri huyo ameipongeza TAWJA na kuahidi kuendelea kuipa ushirikiano, kwa kuwa sehemu ya mabadiliko haya ya kidijitali kuwa ni mabadiliko yenye tija katika kutoa haki ya kijinsia.

“Mmepeleka sheria kutoka kwenye viunga vya Mahakama hadi kwenye jamii kwa kufanya yafuatayo, kuchangia katika uundaji na marekebisho ya sheria zinazolinda wanawake na watoto dhidi ya Ukatili wa Kijinsia (GBV), kuhakikisha sheria zetu ni za haki, jumuishi, na zinawalinda walioko hatarini,” amesema.

Jitihada nyingine zilizofanywa na Chama hicho ni pamoja na kupinga ubaguzi katika mali za ndoa na faragha kupitia sayansi ya sheria yenye msingi wa jinsia; kuwajengea uwezo wasichana na kuonesha kwamba uongozi katika tanuru la haki kupitia Mahakama unawezekana na kuandaa shughuli za jamii ili kuhakikisha Mahakama mtandao inafika hadi maeneo ya pembezoni ambayo ni maeneo ya vijijini.

Kongamano hilo limehudhuriwa na Washiriki mbalimbali ikiwa ni pamoja na Wanachama wa TAWJA kutoka matawi mbalimbali, Wjumbe Waalikwa wa TAWJA, Washirika wa Maendeleo na Wawakilishi wa Jamii ya Kiraia.

✍️mahakama ya Tanzania






Chapisha Maoni

0 Maoni
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.
Chapisha Maoni (0)

#buttons=(Accept !) #days=(20)

Our website uses cookies to enhance your experience. Learn More
Accept !
To Top