Serikali, Diaspora kuimarisha huduma za afya nchini

0


Na Mwandishi Wetu, WAF – Uingereza

Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Dkt. Seif Shekalaghe, amewahimiza Watanzania wanaoishi nje ya nchi (Diaspora) kuendelea kushirikiana na Serikali ili kuboresha na kuimarisha huduma za afya nchini.

Dkt. Shekalaghe ametoa wito huo Machi 16, 2026, wakati wa mkutano uliowakutanisha Watanzania wanaoishi nchini Uingereza pamoja na wale walioko katika nchi nyingine ambao ulifunguliwa kwa njia ya mtandao na Naibu Waziri wa Afya, Dkt. Florence Simazi, lengo ni kutoa taarifa ya utekelezaji wa vipaumbele vya sekta ya afya katika kuhakikisha dhamira ya Afya kwa Wote inafikiwa nchini.

“Ushirikiano huu unalenga kuboresha ubora wa huduma za afya nchini pamoja na kuimarisha huduma za ubingwa na ubingwa bobezi,” amesema Dkt. Shekalaghe.

Aidha, amesema kuwa mkutano huo ni mwendelezo wa mikutano ambayo Wizara ya Afya imekuwa ikiandaa kwa kushirikiana na Ubalozi wa Tanzania nchini Uingereza, kwa lengo la kuimarisha ushirikiano kati ya Serikali na Watanzania wa Diaspora katika maendeleo ya sekta ya afya.

Kwa mujibu wa Dkt. Shekalaghe, kupitia jukwaa hilo mafanikio mbalimbali yamepatikana, ikiwemo kufikiwa kwa makubaliano ya ushirikiano (MoU) kati ya Serikali ya Tanzania na Serikali ya Uingereza. Makubaliano hayo yamewezesha utekelezaji wa miradi na programu mbalimbali za afya kwa ushirikiano wa nchi hizo mbili.

Katika mkutano huo, washiriki walifikia maazimio kadhaa, ikiwemo kuimarisha ushirikiano kati ya Wizara ya Afya na Diaspora katika maeneo yenye matokeo ya haraka, kuendeleza mafunzo na kuwajengea uwezo wataalamu wa afya, pamoja na kuimarisha juhudi za kuanzisha viwanda vya bidhaa za afya nchini, kuimarisha ushirikiano kati ya taasisi za afya za Tanzania na zile za Uingereza.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Shirika la Afya Duniani (WHO) Kanda ya Afrika, Prof. Mohammed Janabi, amesisitiza umuhimu wa Watanzania wa Diaspora kuwa na dhamira ya dhati katika kusaidia kuimarisha huduma za afya nchini, hususan kwa kuwekeza nguvu katika kuboresha huduma za afya ya msingi.

Prof. Janabi amesema ni muhimu pia kuhakikisha maazimio yanayofikiwa katika mikutano kama hiyo yanatekelezwa kikamilifu ili kufikia malengo yaliyokusudiwa.

Mkutano huo umehudhuriwa na viongozi mbalimbali akiwemo Balozi wa Tanzania nchini Uingereza, Mbelwa Kairuki, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya anayeshughulikia vifaa tiba, Bw. Emmanuel Tayari, Mganga Mkuu wa Serikali, Dkt. Grace Magembe, pamoja na viongozi kutoka taasisi za sekta ya afya ikiwemo MSD, TMDA na Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS).

Katika hatua nyingine akiwa nchini Uingereza, Dkt. Shekalaghe anatarajiwa pia kushiriki katika Mkutano wa Global Health Summit, unaowakutanisha wadau mbalimbali wa sekta ya afya duniani.

✍️wizara ya afya








Chapisha Maoni

0 Maoni
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.
Chapisha Maoni (0)

#buttons=(Accept !) #days=(20)

Our website uses cookies to enhance your experience. Learn More
Accept !
To Top