Mradi wa ujenzi wa skimu ya umwagiliaji ya Mwamkulu katika Manispaa ya Mpanda unatekelezwa kwa gharama ya shilingi bilioni 33.9, ukilenga kuongeza uzalishaji wa mazao ya kilimo cha mpunga na mahindi.
Hayo yameelezwa na Naibu Waziri wa Kilimo Mhe. David Silinde (Mb) tarehe 16 Machi 2026, mjini Mpanda wakati wa kuhitimisha ziara ya kikazi ya Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb) ya siku 4 mkoani Katavi.
Mhe. Silinde amesema kuwa kuhusu skimu ya umwagiliaji ya Mwamkulu katika Manispaa ya Mpanda inagharimu shilingi bilioni 33.9 na mradi huo upo kwa asilimia 70, ambapo ujenzi wa bwawa pia utafanyika katika eneo hilo ili kuhakikisha upatikanaji wa maji ya umwagiliaji kwa uhakika.
Kuhusu utozaji ushuru wa mazao, Mhe. Silinde ameeleza kuwa maelekezo ya Serikali ni kuwa wananchi wote wanaotoa mazao mashambani mwao chini ya tani moja kwa ajili ya matumizi ya nyumbani na sio kwa biashara hawapaswi kutozwa faini yoyote ya mazao, hivyo halmashauri kuhakikisha wanasimamia hilo.
Aidha, Mhe. Silinde ameeleza kuhusu upangaji wa bei ya Tumbaku kuwa bei hizo hupangwa kwa kuzingatia gharama anazotumia mkulima katika uzalishaji pamoja na hali ya soko la Dunia, na kuwa mchakato huo hufanyika kwa kushirikisha wadau mbalimbali ili kuhakikisha mkulima anakuwa mnufaika mkubwa wa mazao yake.
Pia, Mhe. Silinde amepokea maelekezo ya Waziri Mkuu Nchemba ya kuhakikisha kuwafuta viongozi wote wa chama cha msingi cha Ilangu AMCOS walioiba fedha za mbolea katika msimu wa kilimo 2024/2025, na kuwa viongozi hao hawapaswi kuwa viongozi licha ya kuwa wamerejesha fedha hizo.
✍️wizara ya kilimo


