Wadau Wajadili Utekelezaji wa Mradi wa tirp2 Kudhibiti Mafuriko na Kulinda Miundombinu ya Reli

0


 Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo anayesimamia Umwagiliaji na Zana za Kilimo, Mha. Athumani Kilundumya, amewataka wadau wanaotekeleza Mradi wa TIRP2 kujadili kwa kina na kwa ufanisi hatua madhubuti za kudhibiti mafuriko yanayoathiri miundombinu ya reli ya kisasa (SGR) na reli ya zamani (MGR), ili kunusuru uwekezaji mkubwa wa Taifa na kulinda maisha ya wananchi.

Mha. Kilundumya ametoa wito huo tarehe 16 Februari 2026, jijini Dodoma wakati akifungua kikao kazi cha wadau kilicholenga kupitia maendeleo ya mradi huo na kuweka mikakati ya kuimarisha utekelezaji wake, ambapo amesema mradi huo awali ulipanga ujenzi wa mabwawa sita, lakini matokeo ya upembuzi yakinifu yamebaini kuwa mabwawa 10 yanahitajika ili kutoa suluhisho la kudumu na la kimkakati dhidi ya mafuriko yanayoharibu miundombinu ya reli na kusababisha hasara za mara kwa mara.

Ameongeza kuwa hatua hii inaashiria mabadiliko makubwa kutoka katika ukarabati wa kawaida hadi suluhisho la muda mrefu lenye uwezo wa kustahimili mafuriko kwa zaidi ya miaka 1,500.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Taifa ya Umwagiliaji (NIRC), Bw. Raymond Mndolwa, amesema utekelezaji wa mradi huo utazingatia vipaumbele kwa kuyapa nafasi ya kwanza mabwawa yenye mchango mkubwa zaidi katika kupunguza mafuriko, ili kuhakikisha rasilimali na bajeti vinatumika kwa ufanisi.

Kikao hicho kilihusisha viongozi na wataalamu kutoka Wizara ya Kilimo; Tume ya Taifa ya Umwagiliaji (NIRC); Wizara ya Maji, Wizara ya Fedha; Shirika la Reli Tanzania; Ofisi za Mikoa ya Morogoro na Dodoma; pamoja na Mshauri Elekezi aliyefanya upembuzi yakinifu wa mradi.

Mradi wa TIRP2 unahusisha ujenzi wa mabwawa sita, pamoja na kuangalia mabwawa mbadala ambayo yatazuia na kupunguza athari za mafuriko kwenye miundo mbinu ya reli, hatua ambayo pia ilikuwa ikisababisha maafa.

Chapisha Maoni

0 Maoni
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.
Chapisha Maoni (0)

#buttons=(Accept !) #days=(20)

Our website uses cookies to enhance your experience. Learn More
Accept !
To Top