Na WAF, Dar Es Salaam
Serikali ya imeweka dhamira dhati ya kupunguza utegemezi wa dawa na vifaa tiba kutoka nje ya nchi kwa kuimarisha mazingira ya uwekezaji katika Sekta ya Afya.
Kauli hiyo imetolewa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Dkt. Seif Shekalaghe, Februari 6, 2026 jijini Dar es Salaam, kwaniaba ya Waziri wa Afya, Mhe. Mohamed Mchengerwa, wakati wa uzinduzi wa mtambo wa teknolojia ya Laser wa maabara ya upandikizaji mimba ya Kituo cha Kairuki Green IVF.
Uzinduzi huo umeenda sambamba na hafla ya kumbukizi ya miaka 27 tangu kufariki kwa Muasisi wa Taasisi ya Kairuki, Hayati Profesa Hubert Kairuki, pamoja na maadhimisho ya miaka mitatu ya utoaji huduma za uzazi pandikizi katika kituo hicho.
Dkt. Shekalaghe amesema Serikali inatambua mchango wa Taasisi ya Kairuki kwenye kuunga mkono dhamira ya Serikali ya kuwekeza katika uzalishaji wa dawa na vifaa tiba kupitia kiwanda cha Kairuki Pharmaceuticals Industry Limited.
Dkt. Shekalaghe amesema matumizi ya teknolojia ya Laser katika huduma za uzazi pandikizi yataongeza ufanisi na ubora wa huduma, hatua inayochangia utekelezaji wa mkakati wa Wizara ya Afya wa mwaka 2021/22–2025/26 unaolenga kuboresha huduma za afya nchini.
"Huduma za uzazi pandikizi zinazotolewa na Kairuki Green IVF zinasaidia kukabiliana na changamoto ya ugumba kwa Watanzania na wateja kutoka nje ya nchi, hivyo kuchangia na kukuza utalii tiba ambao ni kipaumbele cha Serikali ya Awamu ya Sita", amesema Katibu Mkuu Shekalaghe.
Katika hatua nyingine, Dkt. Shekalaghe ameipongeza taasisi hiyo kwa kuhudumia wanandoa 1,712 tangu kuanzishwa kwake, ambapo asilimia 61.4 wamefanikiwa kupata ujauzito, na kutoa wito kwa vituo vyote vya uzazi pandikizi kuzingatia weledi, miongozo na maadili ya taaluma
chanzo: wizara ya afya






