Na OWM – TAMISEMI
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inaendelea kuonesha dhamira ya dhati katika kuimarisha elimu ya lazima ya miaka kumi kuanzia elimu ya awali hadi kidato cha nne, kwa kuweka mkazo katika ulinzi, usalama na ustawi wa watoto walioko mashuleni.
Kupitia Mradi wa BOOST unaosimamiwa na Ofisi ya Waziri Mkuu – TAMISEMI kwa kushirikiana na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Serikali imeandaa mafunzo maalum yaliyoanza kutolewa kwa wadau wa elimu yanayolenga kukabiliana na changamoto za utoro wa wanafunzi, kuimarisha usalama wa watoto pamoja na kukuza usawa wa kijinsia mashuleni.
Akizungumza wakati wa mafunzo hayo, Mratibu wa Mpango wa Shule Salama kupitia Mradi wa BOOST kutoka Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Bi. Suzana Raphael, amesema awamu ya kwanza ya mafunzo iliwahusisha walimu wa unasihi kutoka shule zilizobainika kuwa na changamoto kubwa ya utoro, mazingira hatarishi ya mapito ya wanafunzi wanapoelekea na kurejea shuleni, pamoja na changamoto ya upatikanaji wa chakula shuleni.
Ameeleza kuwa tafiti mbalimbali zinaonesha kuwa upatikanaji wa chakula shuleni unachangia kwa zaidi ya asilimia 80 katika ufaulu wa mwanafunzi, hasa katika kuongeza uelewa, umakini na uwezo wa kujifunza akiwa darasani.
“Mafunzo haya yamelenga kuwajengea uwezo walimu na viongozi wa shule katika masuala ya ulinzi wa mtoto, uandikishaji na kuhakikisha watoto wanamaliza mzunguko wao wa elimu bila vikwazo, sambamba na kupambana na vitendo vya unyanyasaji wa kijinsia,” amesema Bi. Suzana.
Aidha, kupitia afua ya Mpango wa Shule Salama, Serikali imeona umuhimu wa kuwahusisha walimu wakuu wa shule pamoja na Maafisa Elimu Kata kabla ya utekelezaji wa mpango huo ngazi ya shule, ili kuhakikisha viongozi hao wanakuwa na uelewa wa kina wa majukumu yao katika kusimamia usalama na ustawi wa wanafunzi.
Lengo la mafunzo hayo ni kuhakikisha utekelezaji wa Mpango wa Shule Salama unazingatia maeneo yote ya msingi, ikiwemo mapito salama ya watoto kutoka nyumbani hadi shuleni, umbali wanaoutembea, usalama wa barabarani ikiwemo uwepo wa alama za zebra, pamoja na mchango wa jamii katika ulinzi na malezi ya watoto.
Vilevile, washiriki wa mafunzo wamejengewa uwezo wa kutatua changamoto zinazojitokeza katika jamii, ikiwemo vitendo vya ukatili kama ubakaji na ulawiti dhidi ya watoto, pamoja na changamoto zinazowakabili watoto wanaotoka katika kaya masikini, ili kuhakikisha wanashiriki kikamilifu katika masomo yao.
Mafunzo hayo yamehusisha mikoa ya Dar es Salaam, Pwani, Dodoma, Iringa na Morogoro, yakihusisha jumla ya washiriki 1,424. Mafunzo hayo yanatarajiwa kuendelea katika vituo vingine vitano ambavyo ni Iringa, Tanga, Songea, Mwanza, Tabora na Kigoma.
Kwa upande wake, Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Msowero, Bw. Benezekiel Chirwa kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa, ameipongeza Serikali kwa kuandaa mafunzo hayo, akisema yamewajengea walimu stadi na ujuzi wa hali ya juu katika utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku hususani katika ngazi ya shule na jamii kwa ujumla.
chanzo: Tamisemi







