Na WAF-Dar es Salaam
Naibu Waziri wa Afya, Dkt. Florence Samizi amesema Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, imedhamiria kuhakikisha tabasamu la Watanzania linaendelea kuonekana kwa kuboresha huduma za afya nchini.
Dkt. Samizi amesema hayo jijini Dar es Salaam wakati akimkaribisha Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya anayeshughulikia Dawa na Vifaa Tiba, Bw. Emmanuel Tayari, aliporipoti katika Ofisi Ndogo za Wizara ya Afya.
Amesema kuongezwa kwa Bw. Tayari katika timu ya uongozi wa Wizara kutaongeza nguvu na uimara katika utekelezaji wa majukumu ya Wizara, hususan katika kuhakikisha huduma bora za afya, upatikanaji wa dawa na vifaa tiba unaimarika, na hivyo kuweka tabasamu kwa wananchi.
“Serikali ya Dkt. Samia Suluhu Hassan imelenga kuona Watanzania wanapata huduma bora za afya, jambo litakalowezesha tabasamu la wananchi kuonekana na kudumu, sambamba na kutekeleza azma ya Serikali na Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050,” amesema Dkt. Samizi.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Dkt. Seif Shekalaghe, amesema ujio wa Naibu Katibu Mkuu huyo ni sehemu ya mkakati wa kuimarisha utekelezaji wa majukumu ya Wizara.
Amesema uongozi wa Wizara uko tayari kushirikiana bega kwa bega ili kuhakikisha maelekezo ya Rais yanatekelezwa kwa vitendo na kuleta matokeo chanya kwa wananchi.
Naye Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya anayeshughulikia Dawa na Vifaa Tiba, Bw. Emmanuel Tayari, amesema yuko tayari kuitumikia Serikali na Watanzania kwa bidii ili kuhakikisha tabasamu la wananchi linaimarika kupitia upatikanaji wa dawa na vifaa tiba bora, salama na kwa wakati.
chanzo : wizara ya afya


