Na Aisha Swahibu, WAF - Mwanza
Serikali kupitia Wizara ya Afya, kwa kushirikiana na Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR), imepanga kupanua wigo wa utafiti wa dawa za kutibu ugonjwa wa kichocho kwa watoto wenye umri chini ya miaka miwili lengo ikiwa kupata tathimini zaidi ya dawa juu ya matumizi na bei yake ili itakaposajiliwa iweze kukidhi kundi hilo.
Hayo yameelezwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Dkt. Seif Shekalaghe, Februari 17, 2026, wakati akizindua warsha ya utafiti wa ugonjwa wa kichocho mkoani Mwanza.
Amesema tafiti zimebaini kuwa watoto wenye umri chini ya miaka miwili wanaweza kuambukizwa ugonjwa wa kichocho.
“Hapo awali tulikuwa hatufahamu kuwa ugonjwa wa kichocho unaweza kuwaambukiza watoto chini ya miaka miwili, lakini hapakuwa na dawa maalum za kuwatibu watoto wa umri huu, hivyo utafiti huu umebaini uwepo wa dawa inayoweza kutumika kuwahudumia,” amesema Dkt. Shekalaghe.
Ameongeza kuwa dawa hiyo inatarajiwa kuingizwa katika hatua nyingine ya utafiti baada ya kuthibitika kuwa inatibu na ni salama kwa matumizi, hivyo kwa sasa kinachofanyika ni kupanua wigo wa utafiti ambao utalenga kujua bei itakayotumika kununulia itakayokidhi kwa wananchi.
Amefafanua kuwa dawa hiyo tayari imesajiliwa chini ya Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba Tanzania (TMDA), lakini bado haijaingizwa kwenye Muongozo wa Tiba wa Wizara ya Afya.
Aidha, amesema Serikali imeendelea kuchukua hatua za kuzuia maambukizi ya ugonjwa wa kichocho kwa kutoa elimu kwa jamii na kugawa dawa za kinga-tiba kwa watoto kuanzia umri wa miaka sita.
“Serikali imekuja na mkakati wa kuwapatia dawa watoto walio chini ya miaka miwili kupitia utafiti huu. Utafiti ukikamilika, tutaingiza dawa hii kwenye muongozo wa tiba na kuwakinga watoto hawa dhidi ya kichocho, ili hatimaye tuwe na Taifa lenye afya bora,” amesema.
Dkt. Shekalaghe amewakata wataalamu hao kusimamia utafiti huo ili uweze kutoa majibu yenye weledi na tija kwa wananchi na ameitaka jamii kuendelea kuchukua tahadhari ya kujikinga na ugonjwa huo wa kichocho.
✍️Awizara ya afya










