Wawekezaji Wadogo na Wakati Tanzania Waunganishwa na Fursa za Mitaji na Masoko

0


Wawekezaji wadogo na wa kati Watanzania wamepata fursa muhimu ya kuunganishwa moja kwa moja na vyanzo vya mitaji, masoko pamoja na vivutio mbalimbali vya uwekezaji kupitia jukwaa maalum lililoandaliwa na Chemba ya Taifa ya Biashara, Viwanda na Kilimo Tanzania (TNCC) kwa kushirikiana na Mamlaka ya Uwekezaji Tanzania (TISEZA) na Baraza la Biashara Afrika Mashariki (EABC).

Jukwaa hilo lililofanyika mkoani Arusha, liliwakutanisha wawekezaji wa ndani kwa lengo la kufungua fursa mpya za uwekezaji, kuwaunganisha na taasisi za kifedha, pamoja na kuwapatia mwongozo wa namna ya kupata mitaji kwa ajili ya kukuza mnyororo wa thamani wa bidhaa na huduma zinazozalishwa nchini.

Akizungumza katika mkutano huo, Mkurugenzi Mkuu wa TISEZA, Gilead Teri, aliwahimiza wawekezaji Watanzania kusajili miradi yao ili kupata Vyeti vya Uwekezaji, akieleza kuwa vyeti hivyo vinatoa ulinzi wa kisheria pamoja na vivutio mbalimbali vikiwemo msamaha wa Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) na ushuru wa forodha kwa mashine na vifaa vya uzalishaji.

Kwa upande wa upatikanaji wa mitaji, Benki ya Maendeleo ya Tanzania (TIB) ilieleza dhamira yake ya kuwaunga mkono wawekezaji wadogo na wa kati kupitia mikopo yenye masharti nafuu, hususan kwa miradi ya viwanda na biashara zinazoongeza thamani ya mazao na bidhaa za ndani.

Akizungumza kwa niaba ya benki hiyo, Mkurugenzi wa Mipango wa TIB, Joseph Felix Chilambo, alisema benki hiyo inalenga kuhakikisha changamoto ya ukosefu wa mtaji haiwi kikwazo kwa Watanzania wenye nia ya kuwekeza katika shughuli za uzalishaji na biashara.

Naye Rais wa TNCC, Vicent Minja, alisisitiza kuwa jukumu kuu la chemba hiyo ni kuwaunganisha wawekezaji Watanzania na masoko ya ndani na ya kimataifa. Alibainisha kuwa kupitia mtandao mpana wa TNCC, mwekezaji mdogo kutoka Arusha anaweza kupata washirika wa kibiashara kutoka maeneo mbalimbali duniani, jambo litakalochochea uhamishaji wa teknolojia, kuongeza ufanisi na kuimarisha ushindani katika uzalishaji.

Kwa upande wake, Afisa Mtendaji wa EABC, Iman Kajula, alisema jukwaa hilo ni fursa muhimu kwa wawekezaji wengi wa Kitanzania, hasa wale wanaokabiliwa na changamoto ya kutambua na kufikia fursa mpya za uwekezaji. Aliongeza kuwa mkutano huo umefungua milango kwa wafanyabiashara kujifunza, kuunganishwa na wadau sahihi na kuchukua hatua za vitendo za kuanzisha au kupanua uwekezaji wao.

chanzo: Tiseza

Chapisha Maoni

0 Maoni
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.
Chapisha Maoni (0)

#buttons=(Accept !) #days=(20)

Our website uses cookies to enhance your experience. Learn More
Accept !
To Top