Na Ghati Msamba-Musoma
Naibu Waziri wa Kilimo na Umwagiliaji, David Silinde, amesema Serikali inaendelea kuimarisha mifumo ya chakula kupitia Programu ya Mifumo Himilivu ya Chakula (TFSRP) inayotekelezwa nchi nzima katika mwaka wa fedha 2025/2026.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa vifaa vya kisasa vya kilimo cha umwagiliaji, Silinde amesema lengo la Serikali ni kuhakikisha wakulima wanapata zana, teknolojia na maarifa sahihi yanayohimili mabadiliko ya tabianchi na kuongeza tija ya uzalishaji
“Serikali imelenga kukuza sekta ya kilimo kwa asilimia 10 ifikapo mwaka 2030. Tayari miradi 20 imeshaidhinishwa katika awamu ya kwanza kwa mikoa ya Dodoma, Manyara, Tabora, Geita, Lindi na Mara,” amesema Silinde.
Mradi huo unatarajiwa kugharimu Dola milioni 300 za Kimarekani, ukilenga kuongeza uzalishaji kupitia, pembejeo za ruzuku mbegu bora, upimaji wa afya ya udongo, teknolojia za kisasa namiradi mikubwa ya umwagiliaji.
Aidha, Serikali imepanga kujenga skimu za umwagiliaji zitakazonufaisha wakulima wadogo katika mikoa 15, wilaya 45, majimbo 65 na zaidi ya wakulima 4,000 .
Kwa upande wake, Mratibu wa TFSRP – Timotheo Semuguruka, amesema mradi huo unalenga kuboresha huduma za ugani, uzalishaji wa mbegu bora, matumizi sahihi ya maji ya juu na chini ya ardhi pamoja na kuhifadhi chakula na rutuba ya udongo.
“Rais anasisitiza matumizi sahihi na endelevu ya rasilimali tulizonazo, ikiwemo Ziwa Victoria,” amesema Semuguruka.
Naibu Meya wa Manispaa ya Musoma, Haji Mtete, alimshukuru Naibu Waziri kwa ziara hiyo, akisema itasaidia kuongeza uzalishaji, kipato cha wakulima na usalama wa chakula.
Awali, Kaimu Mkurugenzi wa Manispaa ya Musoma – Aines Kamugisha, amesema wakulima 1,127 tayari wamesajiliwa kwenye mfumo wa kidijitali (E-system) kwa ajili ya kupata mbolea, mbegu na ushauri wa kitaalamu mtandaoni. Aidha, vikundi 8 vimewezeshwa kwa vifaa vya kisasa vya umwagiliaji kwa uzalishaji wa mbogamboga na matunda .





