Serikali kupitia Wizara ya Kilimo, kwa kushirikiana na Taasisi na Bodi mbalimbali, imeendelea na zoezi kubwa la ukusanyaji wa sampuli za udongo katika mikoa ya Lindi na Mtwara, zoezi lililoanza rasmi tarehe 9 Januari 2025 na linaendelea hadi sasa.
Sambamba na mikoa hiyo, zoezi hilo pia linafanyika katika mikoa ya Tanga, Morogoro, Tabora na Pwani, ikiwa ni sehemu ya mpango wa Kitaifa wa kupima na kutathmini afya ya udongo nchini.
Zoezi hili linahusisha wataalamu kutoka Wizara ya Kilimo; Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI); Bodi ya Nafaka na Mazao Mchanganyiko (CPB); Bodi ya Mkonge Tanzania; Chuo cha Sukari cha Taifa; Vyuo vya Mafunzo ya Kilimo (MATI); Maafisa Kilimo wa Serikali za Mitaa; Wataalamu kutoka Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine (SUA); Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA); pamoja na wahitimu kutoka vyuo mbalimbali nchini.
Akizungumza wakati wa utekelezaji wa zoezi hilo, mmoja wa wataalamu kutoka Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine (SUA) Prof. Boniface Massawe amesema kuwa lengo kuu ni kuandaa ramani ya afya ya udongo itakayobainisha hali halisi ya rutuba ya udongo katika maeneo mbalimbali ya nchi. Ramani hiyo itasaidia kubaini mazao yanayofaa kulimwa katika kila eneo kulingana na sifa za udongo pamoja na matumizi ya mbolea husika, hali ambayo itawawezesha wakulima kufanya maamuzi sahihi ya kilimo na kuongeza tija na uzalishaji.
Hadi sasa, jumla ya mikoa 13 nchini imefikiwa na zoezi hilo la upimaji wa afya ya udongo, hatua inayotajwa kuwa ni mafanikio makubwa katika utekelezaji wa mpango wa kuboresha sekta ya kilimo, zoezi hili ni chachu ya mapinduzi ya kilimo, kuongeza uzalishaji wa mazao ya chakula na biashara.
chanzo: wizara ya kilimo


