Serikali imedhamiria kuimarisha uzalishaji wa bidhaa za afya (dawa, chanjo, vifaa tiba) na kukuza uwekezaji wa viwanda wa bidhaa hizo hapa nchini hatua itakayochangia kuimarisha upatikanaji wa bidhaa hapa nchini na kuifanya Tanzania kuwa miongoni mwa wazalishaji vinara kwa ukanda wa Afrika.
Hayo yamebainishwa na Waziri wa Afya Mhe. Mohamed Mchengerwa leo Januari 15, 2026 akizungumza mbele ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Afya na Masuala ya UKIMWI Bungeni jijini Dodoma.
“Serikali ya awamu ya Sita chini tmya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imejipanga kuimarisha uzalishaji wa ndani wa dawa, chanjo na vifaatiba, na hapa tumejipanga kuja na mabadiliko makubwa yatakayochangia kuongezeka kwa wawekezaji wa viwanda vya dawa nchini” amesema Mhe. Mchengerwa.
Waziri Mchengerwa amesema kuwa hadi sasa Tanzania inazalisha bidhaa za dawa kwa asilimia 20 pekee huku asilimia 80 za mahitaji tukitegemea kutoka nje ya nchi.
Amesema kwa kuliona hilo, Serikali imejipanga kuvutia wawekezaji wa viwanda vya dawa, chanjo na vifaa tiba kuwekeza nchini ambapo soko la uhakika wa bidhaa hizo lipo ndani na hata nje ya mipaka ya Tanzania.
“Tayari tumeshawakaribisha wawekezaji wenye nia kupitia ‘Call for Expression of Interest’ kupitia Balozi zetu zaidi ya 20, na tunaendelea kupokea maombi ya waekezaji wa viwanda hivyo” amefafanua Waziri Mchengerwa.
Hatuna kiwanda cha chanjo hapa nchini, hii nifursa pia kwa wawekezaji wa viwanda cha chanjo kuja nchini kuwekeza na kuimarisha upatikanaji wa chanjo kwa uhakika zaidi hapa hapa nchini.
Amesema uzoefu uliopatika kipindi cha janga la Ugonjwa wa UVIKO-19 ambapo nchi nyingi zilifunga anga zao, uzalishaji ulipungua huku mahitaji yakiongezeka ulileta changamoto ya upatikanaji wa bidhaa za afya hivyo kuzorotesha katika ustawi wa afya za wananchi wenye uhitaji wa huduma za tiba na kinga hivyo wakati ni sasa kwa Tanzania kujipanga kuongeza uzalishaji wa ndani ya nchi.
Kwa upande wake Mwenyekiti Kamati ya Bunge ya Afya na Masuala ya UKIMWI Mhe. Johannes Lukumay ameipongeza Serikali kwa juhudi inazoendelea kuzichukua katika kuimarisha upatikanaji wa huduma bora za matibabu na kinga kwa wananchi.
Amesema hatua ya Serikali kuimarisha uwekezaji wa VIwanda vya dawa na vifaa tiba ina dhamira njema ya kuhakikisha Watanzania wanakuwa na uhakika wa uwepo wa bidhaa hizo na kufungua soko la kwa mataifa mengine.
chanzo wizara ya afya








