Na Saidi Saidi-WMJJWM – Dodoma
Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima, amesisitiza umuhimu wa kuimarisha ushirikiano kati ya Serikali na wadau mbalimbali, wakiwemo Shirika la Plan International Tanzania, katika kutokomeza ukatili dhidi ya wanawake na watoto na kuimarisha malezi chanya katika jamii.
Dkt. Gwajima amesema hayo Januari 27, 2026 jijini Dodoma wakati wa mazungumzo na Mkurugenzi Mkaazi wa Plan International Tanzania, Bi Jane Sembushe, yaliyolenga kutathmini maeneo ya ushirikiano na kuweka mwelekeo wa pamoja wa utekelezaji.
Dkt. Gwajima amesema Plan International imekuwa mshirika muhimu wa Serikali katika utekelezaji wa Mpango Kazi wa Taifa wa Kutokomeza Ukatili dhidi ya Wanawake na Watoto (MTAKUWAA), Ajenda ya Kitaifa ya Uwekezaji kwa Vijana Balehe (NAIA), pamoja na kampeni za usawa wa kijinsia na uongozi wa mtoto wa kike kupitia mpango wa Girls Takeover.
“Ulinzi wa watoto na uwezeshaji wa wanawake na makundi maalum si jukumu la Serikali pekee, bali ni wajibu wa kila mdau katika jamii.” amesema Dkt. Gwajima
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkaazi wa Plan International Tanzania, Jane Sembushe, amesema Shirika hilo linaendelea kuimarisha ushirikiano na Serikali kwa kuzingatia vipaumbele vya kitaifa, hususan katika maeneo ya ulinzi wa watoto, kutokomeza mila na desturi zenye madhara, kukuza malezi chanya pamoja na uwekezaji kwa watoto na vijana balehe.
Sembushe ameongeza kuwa shirika hilo litaendelea kushirikiana na Wizara katika kuimarisha uelewa wa jamii, ufuatiliaji wa utekelezaji wa programu na kuhamasisha wadau wengine kuunga mkono juhudi za Serikali, akisisitiza kuwa mustakabali wa taifa unategemea ulinzi, malezi bora na uwezeshaji wa watoto wa Kitanzania.
Naye Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Mtoto, Sebastian Kitiku, amesema Wizara inaendelea kuratibu utekelezaji wa afua za malezi na matunzo ya watoto kwa kuzingatia viwango vya kitaifa vilivyoandaliwa, akisisitiza umuhimu wa ushirikiano wa wadau katika kuimarisha uelewa wa jamii na ufuatiliaji wa utekelezaji wa MTAKUWAA.
chanzo: maendeleo ya jamii









