Na WAF, Dar es Salaam
Watoa huduma za afya katika vituo vya umma wametakiwa kufanya mapitio ya mara kwa mara ya ufanisi wa mifumo ya TEHAMA iliyofungwa katika vituo hivyo ili kuhakikisha inatumika kikamilifu na kuleta tija ya ubora wa huduma za afya nchini.
Hayo yamebainishwa na Naibu Waziri wa Afya Dkt. Florence Samizi kwa niaba ya Waziri wa Afya Mhe. Mohammed Mchengerwa leo Desemba 18, 2025 katika kikao cha ushirikishwaji wa wadau kuhusu maandalizi ya utekelezaji wa Sheria ya Bima ya Afya kwa Wote kwa awamu kilichofanyika Jijini Dar es Salaam.
“Serikali haitavumilia vituo vyenye mifumo ya TEHAMA inayotumika kwenye eneo la usajili pekee huku maeneo mengine ya huduma yakiachwa bila matumizi ya mifumo hiyo” amesema Dkt. Samizi na kusisitiza kuwa hali hiyo inachochea kuzotota kwa huduma za matibabu, udanganyifu na kusababisha upotevu wa mapato ya Serikali.
Katika hatua nyingine Dkt. Samizi amewataka watendaji ndani ya Sekta ya afya kuhakikisha kuwa elimu ya bima ya afya kwa wote inaendelea kutolewa katika vituo vya kutolea huduma za afya, ili wananchi wanaokuja kupata huduma waweze kuelewa haki zao na huduma wanazostahili kuzipata kulingana na michango wanayolipa.
Naibu Waziri huyo amesisitiza kuwa utoaji wa elimu kwa upole na kwa usahihi utasaidia kuongeza uelewa kwa wananchi, kuboresha utoaji wa huduma na kuimarisha uaminifu kati ya Serikali na wananchi.








