Na Angela Sebastian
Bukoba : Viongozi wa dini mkoani Kagera wamewataka viongozi wa Serikali kuandaa mijadala ya mara kwa mara kati yao ili kukutana na kuongea namna ya kuzitatua changamoto zinazoweza kujitokeza na kusababisha uvunjifu wa amani ambayo ni Tunu ya Taifa letu.
Viongozi hao wameeleza hayo leo wakati wa Dua na sala ya kuombea Taifa na mkoa huo katika uzinduzi wa kongamano la Ijuka Omuka (Kumbuka nyumbani)lililoandaliwa na mkuu wa mkoa wa Kagera Hajat Fatma Mwassa kwa lengo la kutangaza fursa za kiuchumi zilizipo mkoani humo.
Shekh Abdulshahid Abbas ni kiongozi wa Answari Suna amesema viongozi wa dini wamepewa dhamana ya kuhakikisha tunapeleka watu mbinguni na siyo motoni na mwalimu mzuri ni yule anayefundisha wanafunzi wake kulinda amani ya nchi yao pia wazazi wazuri ni wale wasiosahau wajibu wao wa malezi kwa watoto.
Alisema vitabu vyote vya dini vinahimiza watu kuwa wamoja,kupenda nchi zao,kutohasi mema tunayojaaliwa na Mungu maana hakuna shetani mbaya kama mtu anayehimiza mihemko kwa vijana eti Gen-z waende kuharibu rasilimali za nchi yao kutokana na uchochezi wa watu wabaya wasiotutakia mema.
"Nawashauri viongozi wa Serikali kuweka utaratibu wa kutuita na kukaa pamoja mara kwa mara ili kuweka mambo sawa ambayo yanatatiza watu wetu kabla hayajaleta madhara yanayoweza kuliangamiza Taifa letu pia silaha kubwa ya kumaliza mambo pale inapotokea taharuki ni vyema kunyamza na kumuomba Mungu kwani hiyo ndiyo busara"
Alisema cheo ni dhamana Mungu alitupatia nafasi ya kulea watu wake na kushauri viongozi pale wanapokosea tuwapeleke pembeni na kuwashauri siyo kuwaanika.
Padre Philibart Mutalemwa mkuu wa idara ya utume na walei jimbo katoriki la Bukoba alisema na Mchungaji Ayub Silvester wa madhehebu ya CPCT wamewaombea wanakagera na watanzania kulinda amani ya nchi yetu,kuondokana na moyo wa kubaguana kwa njia yoyote ikowemo udini ukabila na jinsia bali wapendane na kuheshimiana pia wasiruhusu watu kuwachonganisha kwa njia yoyote.
Kwa upende wa mkuu wa mkoa huo Hajat Fatma Mwassa akifungua kongamano hilo baada ya dua na sala za viongozi mbalimbali wa dini aliwashukuru wananchi wa mkoa huo kwa kuonyesha uzalendo wakati wa kampeni, uchaguzi na baada ya uchaguzi mkuu mwaka huu kwani ni jambo la kuigwa.
""Wanakagera waliisha onja machungu ya uvunjifu wa amani kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo vita ya Kagera ya mwaka 1978 na matukio mengine kama vile ugonjwa wa HIV,ajali ya Meli ya Mv Bukoba na ndege zilizochukua maisha ya watu wengi hali ambayo ilirudisha maendeleo ya mkoa huu nyuma hivyo waliona ni vyema kujiepusha na uvunjifu wa amani nawashukuru na kuwapongeza sana"alisema Mwassa
Aliwataka wanakagera kutokubali kuwagawa kwa njia yoyote ile hususani udini,ukabila wala utu wa mtu kwani mhasisi wa Taifa hili mwalimu Julius Kambarage Nyerere alikemea kwa nguvu zote hivyo hata mimi nitalikemea kwa nguvu zangu zote kwani mtu akileta hoja ya kuvunja umoja wetu na kutugawa tumwambie huo ni udhaifu.










