Tanzania na Malawi Kushirikiana Katika Biashara ya Mahindi

0


Tanzania imeihakikishia Malawi kuwa iko tayari kushirikiana nayo katika biashara ya mahindi kulingana na mahitaji ya nafaka hiyo. 

Hayo yamesemwa na Dkt. Stephen J. Nindi, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo anayesimamia Maendeleo ya Mazao na Usalama wa Chakula kufuatia mazungumzo yake na Bi. Erica Maganga, Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo ya Malawi tarehe 17 Desemba 2025, jijini Lilongwe, nchini Malawi.

Dkt. Nindi alieleza kuwa Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) ina akiba ya zaidi ya tani 500,000 za mahindi, hivyo Tanzania iko tayari kuendeleza mahusiano ya kibiashara na Malawi kulingana na mahitaji. Kwa upande wake, Bi. Maganga aliipongeza Tanzania kwa mifumo yake ya hifadhi ya nafaka kwa kueleza kuwa inazingatia viwango vya ubora.

Viongozi hao walijadili pia fursa za kuimarisha biashara ya mahindi na ushirikiano wa kukabiliana na changamoto za usalama wa chakula unaochangiwa na mabadiliko ya tabianchi.

Katika hatua nyingine, ujumbe wa Tanzania ulikutana na uongozi wa NFRA ya nchini Malawi pamoja na uongozi wa Chama cha Wauzaji na Wasindikaji wa Nafaka cha Malawi (GTPA) na kujadili fursa za kibiashara za zao la mahindi, masuala ya udhibiti wa sumukuvu na changamoto za masoko.

Washiriki wengine katika ujumbe wa Tanzania  ni pamoja na Dkt. Andrew Komba, Afisa Mtendaji Mkuu wa NFRA; Bw. Robinson Meitinyiku, Mjumbe wa Bodi ya Ushauri ya NFRA; na Mhe. Agnes Kayola, Balozi wa Tanzania nchini Malawi.

Chapisha Maoni

0 Maoni
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.
Chapisha Maoni (0)

#buttons=(Accept !) #days=(20)

Our website uses cookies to enhance your experience. Learn More
Accept !
To Top