Na Angela Sebastian
Bukoba : MBUNGE wa Jimbo la Bukoba Mjini mkoani Kagera Mhandisi Johnston Mutasingwa,amewashauri waandishi wa habari wa Manispaa ya Bukoba kuibua habari za uchambuzi juu ya changamoto zinazowakabili wananchi ili zijulikane na kutafutiwa ufumbuzi wa kina.
Pia amewaomba watoe ushirikiano kwa viongozi walioko madarakani kisha kuitangaza miradi ya maendeleo iliyotekelezwa na inayoendelea kutekelezwa kwa kuandika habari za mwendelezo ili jamii itambue miradi hiyo imefikia hatua gani na faida zake ni zipi kwasababu, inatekelezwa kutokana na kodi za wananchi.
Mutasingwa amesema hayo leo wakati akizungumza waandishi habari mjini Bukoba na kusema kwamba, umuhimu wa ushirikiano huo ni kuhakikisha kuwa habari zinazotolewa zinasaidia jamii kupata taarifa sahihi na za kina kuhusu miradi mbalimbali ya maendeleo.
"Nyie ni wanataaluma ya habari tutumie kalamu zetu kuibua habari zenye kuvutia wasomaji na watazamaji,tuwe na mwendelezo mfano, umeandika habari inayohusu ujenzi wa soko fuatilia mpaka mwisho ili wasomaji wapende kusoma,kusikiliza na kuangalia maana,habari yenye mwendelezo inashawishi mtu aendelee kuifuatilia"ameeleza Mutasingwa.
Amesema habari kama hizi zitachangia vyombo vyetu vya habari na waandishi wake kuongeza kipatao kwasababu ikiwa ni gazeti wananchi watahakikisha wananunua magazeti ili wasome kinachoendelea,mitandaoni lazima watafungu,radio watasikiliza na Televisheni wataongeza watazamaji na wasilizaji wengi.
Aidha amewataka kutumia kalamu zao kuandika habari zenye kuchochea Amani kwasababu bila amani maendeleo hayawezi kupatikana.
Amani Kajuna ni mkazi wa mkoa wa Kagera ambaye pia alikuwa kampeni meneja wa mbunge huyo amesema waandishi wa habari ni kioo cha jamii,ni macho ya viongozi na wananchi,ni sauti ya jamii nzima ya Taifa la Tanzania hivyo, ni vyema viongozi wakashirikiana na waandishi kwani safari ya siasa inalenga maendeleo kwahiyo inahitaji ukaribu wa pamoja.






