Mdeme Ahimiza Wanawake Kuwekeza Nguvu Kwenye Malezi ya Watoto

0


Na Abdala Sifi WMJJWM- Pwani 

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Felister Mdemu ametoa wito kwa Wanawake kuwekeza nguvu katika malezi ya Watoto wao ili kuhakikisha wanakua katika maadili mema.

Mdemu amesema hayo Desemba 19, 2025 alipotembelea vikundi vya Wanawake na Vijana Wilaya ya Kisarawe Mkoani Pwani kwa lengo la kujionea shughuli za uzalishaji katika miradi yao inayotokana na mikopo ya asilimua kumi inayotolewa na Halmashauri pamoja na mfuko wa maendeleo ya wanawake unaotolewa na Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum

Pamoja na kuvipongeza vikundi hivyo, Mdemu amewasisitiza Wanawake kwamba, malezi bora ya watoto ni msingi wa maadili mema, utu pamoja na ulinzi dhidi ya ukatili wa aina yoyote hali itakayochangia kuongeza fursa za ubunifu na uzalishaji kiuchumi.

“Nimefurahishwa na ubunifu wa shughuli zenu nawapongeza kwa kazi nzuri, niwaombe muendelee kuwapa wengine elimu ya fursa zinazotolewa na Serikali chini ya Uongozi wa Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, ambaye ameweka mazingira rafiki ya wanawake na Vijana kuinuka kiuchumi" amesema Mdemu.

Awali, akitoa maelezo ya awali, Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe Mhe. Petro Magoti amesema elimu kuhusu fursa mbalimbali inaendelea kutolewa kwa Wanawake na Vijana ambapo vikundi vya Wanawake ikiwemo wajane zaidi ya mia tatu (300) wanaendelea kujengewa uwezo kwa kupewa vifaranga kwa ajili ufugaji.

Ameongeza kwamba ili kuongeza tija kwa Vijana Wilaya ya Kisarawe imetenga maeneo maalum kwa ajili  Wanawake na Vijana kuendesha shughuli za kiuchumi.

Mmoja wa wanakikundi cha Upendo, kinachoendesha shughuli za uongezaji thamani, ikiwemo kubangua korosho, uchakataji wa mbogamboga na ukamuaji wa mafuta ya alizeti Lydia Jackob ameishukuru Serikali kwa kuendelea kuwezesha Wanawake kiuchumi huku akitoa hamasa kwa Wanawake wengine kuchangamkia fursa hizo.




Chapisha Maoni

0 Maoni
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.
Chapisha Maoni (0)

#buttons=(Accept !) #days=(20)

Our website uses cookies to enhance your experience. Learn More
Accept !
To Top