📌Shamba Darasa la Kijiji cha Mbeere South, Kaunti ya Embu Latajwa kusaidia Wakulima wadogo kuokoa zaidi ya asilimia 40 ya gharama walizokua wanatumia kumwagilia kwa Pampu za Dizeli
WAKULIMA wengi vijijini wanaendelea
kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi, huku teknolojia ya nishati ya
jua ikitajwa kuwa mkombozi katika kupunguza utegemezi wa mvua, kuongeza mavuno
na kuboresha usalama wa chakula na maisha yao.
Hata hivyo, tafiti zinaonyesha matumizi ya teknolojia hii bado ni madogo kutokana na gharama kubwa za vifaa, ubora hafifu wa baadhi ya bidhaa, na ukosefu wa elimu ya kutosha kupitia vyombo vya habari kuhusu faida na matumizi sahihi ya teknolojia hiyo.
Ubunifu wa SowPrecise Africa
Katika kijiji cha Gachuriri, eneo la Mbeere
South kaunti ya Embu, Kenya, wakulima wengi hutegemea mvua au pampu za dizeli
kumwagilia mashamba yao. Eneo hilo lina ukame wa mara kwa mara na mvua
zisizotabirika, hali inayosababisha kilimo cha kubahatisha na gharama kubwa za dizeli
licha ya kuwa na ardhi nzuri na yenye rutuba.
Mwaka 2022 Linda Kamau, Julia Kinuthia na Pius Wambua waliona fursa katika changamoto hizo na kuanzisha kampuni ya SowPrecise Africa inayotumia teknolojia ya umwagiliaji wa jua unaohamishika kupitia mradi wao SunRider. Mfumo huo unalenga wakulima wadogo kwa gharama nafuu, ukiwawezesha kulima mwaka mzima bila kutegemea mvua huku wakitumia chanzo cha maji cha mto Thiba ulio pembenzoni mwa shamba lao.
Linda, Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni hiyo, anasema safari ya kuanzisha shamba darasa hilo lenye ekari 20 haikuwa rahisi kupata fedha, lakini walipofanikiwa kuwasilisha wazo la mradi huo na kufanikiwa kupata fedha za awali dola 10,000 kutoka kwa taasisi ya Allan & Gill Gray Philanthropies (AGGP.
“Baada ya kupata fedha hizo walianza kuonyesha teknolojia hiyo kwa wakulima waliokuwa wakitegemea mvua au pampu za dizeli jinsi tunavyoweza kulima mwaka mzima kwa gharama nafuu na wakulima walianza kuja kujifunza na kushuhudia mafanikio na hivyo kuanza kuhitaji huduma yetu.
Baadaye mwaka 2024 tulifanikiwa kupata tena fedha za ruzuku kutoka Heifer International baada ya kushiriki Shindano la AYuTe ambapo fedha hizo zimesaidia kupanua shughuli za mradi wetu ikiwa ni pamoja na kuongeza mifumo ya sola ili kuwafikia wakulima wengi zaidi” Amesema Linda
Faida za Mashamba Darasa ya Nishati ya Jua
Linda anabainisha kuwa zaidi ya asilimia 80 ya ardhi ya Kenya ni kame, na ni asilimia 2 pekee inayotumika kwa kilimo cha umwagiliaji.
“Teknolojia kama tuliyoanzisha ina mchango mkubwa katika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi hadi sasa, SowPrecise imeunda mifumo ya umwagiliaji inayohudumia wakulima katika maeneo matano, ambapo kila mfumo unaweza kumwagilia hadi ekari 10 kwa siku huku mifumo yetu ikiwa na uwezo wa kusukuma maji kati ya lita 10,000 hadi 50,000 kwa saa
Wakulima hulipa Ksh 1,500 kwa ekari kwa wiki, kupitia mkataba wa mwaka mzima, hali inayowawezesha kulima mara tatu kwa mwaka na kuongeza mapato kwa asilimia 30.” Amesema Linda
Wakulima Waeleza Tofauti Kabla na Baada ya Mradi
Stephen Mutua mkulima wa maharage na mahindi, anasema kabla mradi huo alikua akitumia pampu ya dizeli na alikuwa natumia hadi Ksh 4,500 kwa wiki lakini sasa anatumia solar na kulipia Ksh 1,500 tu na hakuna tena gharama za mafuta au matengenezo.
Janet kwa upande wake anasema kuwa matumizi ya solar katika umwagiliaji ni nafuu zaidi kuliko pampu za mafuta, ingawa gharama za awali za ununuzi kwa vifaa vya Solar bado ni kikwazo kwa wakulima wengi.
Teknolojia ya Solar Isiyotumia Betri
Pius Wambua msimamizi mwenza wa kampuni, anaeleza kuwa solar pumps wanazotumia ni teknolojia ambayo panel za solar hazihitaji betri.
“Paneli hizi hukusanya umeme kutoka juu na
chini, hivyo zinapunguza gharama kwa asilimia 40 ukilinganisha na pampu za
dizeli.
Ni vyema mkulima kabla hajaagiza au kwenda dukani kukunua ni vyema akafanya utafiti na kuwahusisha wataalm huku akishauri kuacha tabia ya kununua vifaa vya ubora wa chini mtandaoni au madukani bila ushauri wa wataalam.
“Ni muhimu kutumia vifaa vilivyoidhinishwa na kupimwa kitaalamu kabla ya kununua ili kuondokana na changamoto wanazopata wakulima wengi ambao wengi wao wanaishia kupata hasara” anasisitiza Pius.
Kwa Nini Matumizi Bado ni Madogo?
Utafiti uliofanywa na Musoma Tv katika Kijiji cha Bugwema wilaya ya Musoma, Mkoani Mara, ulibaini changamoto kuu zikiwemo gharama kubwa za vifaa, ukosefu wa wataalam vijijini, na masharti ya upatikanaji mikopo rafiki kwa wakulima wadogo.
Briton Moris mkulima wa Bugwema, Mara katika mahojiano maalum na Musoma Tv alisema anatumia hadi lita 20 za mafuta kwa siku kumwagilia ekari moja kutokana na ardhi kuhitaji maji mengi na Solar ingesaidia sana, lakini gharama za vifaa ni kubwa.”
Naye Penina Elisha anasema yeye bado anategemea umwagiliaji wa mkono kutokana na kukosa fedha za kununua pampu au mfumo wa solar.
Matumizi ya Solar Zaidi ya Kilimo
Teknolojia ya umeme jua imeleta mapinduzi pia kwenye sekta ya uvuvi katika Ziwa Victoria kupitia mitambo ya kukaushia dagaa kwa nishati ya jua (solar dryers).
Mhandisi Wistone Nnko ni kutoka kampuni ya
Millennium Engineers Mwanza, anasema awali kabla ya kuanzisha mradi wa Solar Dryer katika mwalo wa Kayenze ndogo jijini Mwanza dagaa walikaushwa kwa mchanga au
vichanja, lakini sasa solar dryers hukausha ndani ya saa tatu pekee kwa usafi
na ubora wa kimataifa.
Wafanyabiashara wa dagaa kama Agness Selestine na Latifa Buchoji wanasema teknolojia hii imepunguza upotevu, kuboresha ubora, na kuongeza thamani sokoni.
Ripoti ya Uandishi wa Habari Kuhusu Solar
Kituo cha African Centre for Media Excellence kimekua kikifanya utafiti katika vyombo vya habari katika ripoti zinazohusu matumizi ya nishati ya jua katika kilimo pamoja na kutoa mafunzo kwa waandishi wa habari ili waweze kutoa habari zenye tija kwa jamii ili kuhamasisha matumizi ya nishati hiyo.
Tarehe 20 - 24 Octoba, ACME iliandaa warsha Jijini Nairobi kwa waandishi wa habari 16 kutoka Tanzania, Kenya na Uganda na kutoa elimu kwa waandishi hao, namna Bora ya kuandaa na kuripoti habari zenye tija kuhusu matumizi yenye tija kuhusu nishati ya umeme jua katika kilimo pamoja na kueleza matokeo ya utafiti uliofanyika mwaka 2024 na matokeo ya utafiti huo kutolewa 2025.
Kwa mujibu wa ACME, Ripoti iliyotolewa mwezi May, 2025 matokeo ya utafiti huo yanaonyesha kuwa, Kuna ongezeko la taarifa za vyombo vya habari kuhusu
matumizi ya nishati ya jua katika kilimo kwa asilimia 79 kutoka habari 63 mwaka
2023 hadi 113 mwaka 2024.
Ripoti hiyo inaeleza kuwa bado kuna changamoto ya nafasi ndogo za habari hizi, upungufu wa uchambuzi wa kina, na ukosefu wa uwiano wa kijinsia kwenye vyanzo.
Brian Ssenabulya ni Afisa wa Utafiti wa ACME, anasema habari nyingi zilibaki kwenye mada za umwagiliaji ambazo ni sawa na 67.1% huku masuala kama uhifadhi, uchakataji, na ukaushaji yakipata uangalizi mdogo licha ya umuhimu wake.
Awali akizungumza wakati wa kufungua warsha hiyo iliyofantika katika ukumbi wa Swiss Belinn Hotel Nairobi, Rachel Mugarura-Mutana ambaye ni Meneja wa Programu na Mafunzo kutoka ACME, amesema ni lengo la kituo hicho kuandaa warsha hiyo ni kuwajengea uwezo waandishi
kutumia fikra za mfumo (system thinking) katika kuripoti habari za nishati ya
jua kwa mtazamo wa kijamii, kiuchumi, na kimazingira.
" Mafunzo haya yanatoa fursa kujifunza, kubadilishana uzoefu pamoja na kushirikiana katika kuelimisha jamii juu ya matumizi yenye tija ya nishati ya jua katika kilimo.
Pia kuwawezesha waandishi kufirikiri zaidi ya habari zaidi ya umwagiliaji, uhifadhi,uzalishaji ili kuhamasisha jamii juu ya matumizi ya nishati ya Jua" Amesema Rachel
Mtazamo wa Waandishi Baada ya Mafunzo
Amy Moyi wa Elveza Media (Kenya) amesema amejifunza kuandika habari za nishati kwa mtazamo wa mfumo unaochunguza sababu za msingi, majukumu ya kijinsia, na athari za kijamii na kiuchumi.
“Sasa naweza kuandaa taarifa zinazochochea mjadala na hatua za sera” Amesema Amy
Naye John Okot kutoka Numec (Uganda) amesema mafunzo yamemfundisha kuunganisha mifumo mbalimbali ili kuzalisha habari za kina na zenye athari.
“Nimejifunza kutofautisha uandishi wa
suluhisho na uandishi wa matangazo au mahusiano ya umma,” aliongeza John.















