Wizara ya Kilimo imetoa mafunzo ya Mfumo wa Kidigitali wa kusajili ghala, masoko, vituo vya ukaguzi wa mazao na wafanyabiashara (Crops Stocks Dynamics System) kwa waendesha ghala, Maafisa Ugani, na halmashauri za vijiji mkoani Ruvuma, ili kuongeza ufanisi, uwazi na uwajibikaji katika uendeshaji wa ghala za Umma.
Mafunzo haya pia yameambatana na wadau hao kupatiwa elimu kuhusu Mwongozo wa Uendeshaji na Usimamizi wa Ghala za Umma, ambapo utekelezaji wake unahusisha kutoa taarifa ya kiasi cha mazao yaliyoingia na kutoka kwenye ghala kwa mwaka husika.
Bw. Wycliffer Mulinda-Afisa Mtendaji wa Kata ya Lusewa kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Namtumbo ambaye ni miongoni mwa waliopata mafunzo hayo, amesema mafunzo hayo yatamsaidia kutoa elimu kwa jamii ili iwe tayari kupokea teknolojia za kisasa kupitia vituo vya kutoa huduma za zana za kilimo, ambapo Serikali imelenga kuvianzisha kwa kila kata nchini, ili kuhaulisha teknolojia za kilimo na kutoa huduma za teknolojia za kisasa kwa wakulima katika mnyororo wa thamani wa kilimo.
Naye, Bi. Asha Maokola-Afisa Kilimo wa kata ya Litisha Halmashauri ya Wilaya ya Songea Mkoani Ruvuma amesema, Serikali Kupitia Mwongozo wa Uendeshaji wa Vituo vya kutoa huduma za Zana za Kilimo imeelekeza Halmashauri zote nchini kutenga maeneo kwa ajili ya ujenzi wa vituo vya zana za kilimo kwa kila kata, akisema kata ya Litisha imetenga eneo katika kijiji cha Morogoro kwa ajili ya ujenzi huo.
Pia, Bi. Maokola amesema " Uwepo wa Vituo vya Zana za Kilimo katika kila kata utarahisisha shughuli za kilimo na kuondoa usumbufu utokanao na utegemezi wa jembe la mkono ambapo wakulima hutumia gharama kubwa na muda mrefu katika shughuli za kuandaa mashamba wakati wa msimu wa kilimo na hivyo kuchelewesha shughuli za upandaji na uvunaji zinazopelekea hasara kwa mkulima.”
Mafunzo hayo yametolewa tarehe 16 -17 Oktoba 2025 na kushirikisha pia Watendaji wa Vijiji, Wakuu wa Idara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi kutoka Halmashauri, Maafisa Kilimo Wilaya, Maafisa Kilimo Mkoa, Waendesha ghala, kutoka katika Halmshauri ya Wilaya ya Songea, Madaba, Namtumbo na Songea Manispaa.
Chanzo: wizara ya kilimo


