Mwanasheria Mkuu wa Serikali Mhe. Hamza S. Johari amewataka Mawakili wa Serikali kutumia vizuri mikataba ya PPPC ambayo itasaidia kufanikisha malengo ya Dira Ya Taifa 2050 katika kuboresha maisha na kuongeza kipato kwa wananchi na taifa kwa ujumla.
Mhe. Johari ameyasema hayo tarehe 7 Oktoba, 2025 wakati akifungua mafunzo kwa Mawakili wa Serikali kutoka Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali,yaliyotolewa na Kituo cha Ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi (PPPC) Jijini Dodoma.
Mhe. Johari alimshukuru Mkurugenzi Mkuu na Uongozi wa PPPC kwa kuandaa na kufadhili mafunzo haya kwa Mawakili wa Serikali kwani kupitia mafunzo haya mawakili watapata uelewa wa uandaaji wa miradi ya ubia.
*"Nitoe pongezi za dhati kwa Mkurugenzi Mkuu na Uongozi wa PPPC kwa kuandaa na kufadhili mafunzo haya, ambayo yanalenga kuwajengea uelewa wa kina wa kitaalam pamoja na stadi za kivitendo zinazohitajika katika kusimamia masuala ya mikataba ya ubia." *Amesema Mhe. Johari
Aidha, Mwanasheria Mkuu wa Serikali alitoa wito kwa Mawakili wa Serikali kuwa na ari ya kujifunza na kuwa wabobezi katika mambo mbalimbali.
*"Muwe na ari ya kujifunza ili kuhakikisha mnachukua maarifa haya na kuyaweka katika vitendo, kwani wajibu wetu ni kuhakikisha kuwa PPPC inaendeshwa kwa ufanisi na kwa mujibu wa Sheria na kanuni zilizopo."* Amesema Mhe Johari
Awali, akimkaribisha mgeni rasmi kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa PPPC, Bi. Flora Tenga, Mkurugenzi wa Huduma za Kisheria alitoa shukrani kwa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa kuonesha ushirikiano na kuonesha umuhimu wa mafunzo hayo.
*"Ninawashukuru sana Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, kwa utayari wenu wa kupokea mafunzo haya ,kwani kuna umuhimu sana kwa Mawakili wa Serikali kupata uelewa kiutendaji kupitia mikataba ya ubia."* Amesema Bi. Flora Tenga
Mafunzo kwa Mawakili wa Serikali wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali , yanayotolewa na Kituo cha Ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi (PPPC) yaliyofunguliwa tarehe 7 Oktoba 2025 yataendelea hadi 9 Oktoba, 2025 jijini Dodoma.
Chanzo: ofisi ya mwanasheria mkuu wa serikali