Mbibo Aongoza Kikao cha Wataalam Kujadili Utoroshaji Madini Nchini

0


đŸ‘‰Amesema ni wajibu wa kila Mtanzania kulinda rasilimali za taifa

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Msafiri Mbibo, ameongoza kikao cha wataalam kutoka taasisi mbalimbali za Serikali kwa ajili ya kujadili mikakati ya kudhibiti utoroshaji wa madini nchini.

Kikao hicho kimefanyika Oktoba 7, 2025, katika Ukumbi wa Mikutano wa Wizara ya Madini Mtumba jijini Dodoma.

Akizungumza katika kikao hicho, Mbibo amesema kuwa ni wajibu wa kila Mtanzania kushiriki kikamilifu katika kulinda rasilimali za taifa, hasa madini, kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.

"Utoroshaji wa madini ni tishio kwa uchumi na usalama wa taifa letu. Tunapaswa kushirikiana kwa dhati katika kudhibiti mianya yote inayochangia vitendo hivi," amesema Mbibo.

Aidha, amesema kuwa utoroshaji wa madini umekuwa ukiliingizia taifa hasara kubwa ya mapato, na kwamba ipo haja ya dharura ya kuunganisha nguvu za pamoja katika kudhibiti vitendo hivyo haramu.

“Madini ni miongoni mwa rasilimali muhimu zinazotegemewa katika kuchochea maendeleo ya taifa letu. Hatuwezi kukubali kuendelea kupoteza mapato kwa sababu ya mianya ya utoroshaji. Ni wajibu wa kila mmoja wetu kama watanzania wazalendo  kushiriki katika vita hii,” amesema Mbibo.

Katika kikao hicho, Mbibo ameeleza kuwa Serikali inahitaji kuwa na mfumo thabiti na shirikishi wa udhibiti wa madini kuanzia migodini, kwenye vituo vya ukaguzi, hadi viwanja vya ndege, bandari na mipaka yote ya nchi.

Pia, ametoa wito wa kuundwa kwa timu maalum za kitaifa zenye wataalam kutoka taasisi mbalimbali, zitakazoshirikiana katika kufanya uchunguzi, ufuatiliaji na ulinzi wa madini, hasa katika maeneo ambayo yameonekana kuwa na mianya mikubwa ya utoroshaji.

“Tunapaswa kuwekeza katika vifaa vya kisasa vya kuchunguza na kubaini madini hususan madini ya vito  kwa haraka na kwa uhakika. Vifaa hivi vitasaidia sana kuzuia mbinu mpya zinazotumiwa na wanaojihusisha na utoroshaji,” amesisitiza.

Mbibo pia amependekeza kuanzishwa kwa mpango wa mafunzo endelevu kwa wataalam wanaofanya kazi katika maeneo ya ukaguzi ili kuwajengea uwezo wa kutambua aina mbalimbali za madini, mbinu za usafirishaji haramu na matumizi ya teknolojia ya kisasa katika kudhibiti biashara hiyo haramu.

Katika hitimisho la kikao, wadau walikubaliana kuweka mikakati ya haraka ya utekelezaji wa maazimio yaliyopitishwa, ikiwa ni pamoja na kuandaa mpango kazi wa pamoja utakaohakikisha udhibiti wa utoroshaji wa madini unafanyika kwa ufanisi na kwa muda mrefu.

Kikao hicho kimehusisha ushiriki wa taasisi mbalimbali za Serikali ikiwemo Wizara ya Madini, Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Tume ya Madini, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), pamoja na Mamlaka ya Viwanja vya Ndege (TAA).

Chanzo: wizara ya madini







Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.
Post a Comment (0)

#buttons=(Accept !) #days=(20)

Our website uses cookies to enhance your experience. Learn More
Accept !
To Top