Na Ghati Msamba
Musoma : MKUU wa Wilaya ya Musoma, Juma Chikoka, amewataka wataalamu wa kilimo wa vijiji na kata katika Halmashauri ya Musoma kutumia vitendea kazi (vishikwambi) walivyokabidhiwa kwa malengo yaliyokusudiwa, ili kuongeza ufanisi katika kazi zao kwa kuweka kumbukumbu na taarifa sahihi badala ya matumizi yasiyokusudiwa.
Chikoka alitoa wito huo wakati wa hafla ya makabidhiano ya vifaa hivyo iliyofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Halmashauri ya Musoma.
Amesema lengo la Serikali kutoa vifaa hivyo ni kuhakikisha matokeo yanapatikana ndani ya muda uliopangwa ili kuleta tija katika sekta ya kilimo na mifugo. Aidha, alisema hatua hiyo inalenga kuwezesha upatikanaji wa chanjo kwa gharama nafuu, kuongeza uzalishaji na kuboresha masoko ya mazao ya kilimo na mifugo.
Vilevile, amewataka wataalamu hao kwenda kufanya kazi kwa umakini mkubwa na kuhakikisha wanahamasisha wafugaji kuanzisha vizimbavya samaki na kufuga kuku katika maeneo yao, ili kila mwananchi aweze kushiriki katika uzalishaji mali.
“Rai yangu kwa wananchi, pindi zoezi hili litakapofika katika vijiji vyenu, toeni mifugo yenu ili ipatiwe tiba na chanjo. Pia, mtoeni ushirikiano kwa wataalamu wetu ili wapate takwimu sahihi za idadi ya mifugo, kama tulivyofanya kwa wananchi wa maeneo mengine,” alisema Chikoka.
Mkuu huyo wa Wilaya alimshukuru na kumpongeza Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kwa jitihada kubwa anazozifanya katika kuweka ruzuku kwenye sekta ya kilimo, hatua ambayo imeongeza tija na kuimarisha uzalishaji wa mazao na mifugo nchini.
Kwa upande wake, Mkuu wa Idara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi wa Halmashauri hiyo, Kelvin Ruge, alisema kuwa katika utekelezaji wa mpango wa mwaka 2020/2024, wamefanikiwa kufanya chanjo kwa mifugo kwa kiwango kikubwa.
Alibainisha kuwa halmashauri imepokea vifaa mbalimbali na dawa za chanjo, zikiwemo dozi 110,000 za homa ya mapafu, chanjo za ng’ombe 30, chanjo za “stoka” za kondoo na mbuzi 103,000, chanjo ya “Tatu Moja” dozi 180,000, maboksi 22 ya kuhifadhia dawa, sindano 22, magambuti 13 na vishikwambi 47.
Amesema gharama ya chanjo ya homa ya mapafu kwa ng’ombe ni shilingi 500, huku chanjo ya mbuzi na kondoo ikiuzwa shilingi 300. Kila mfugaji alipewa stakabadhi rasmi ya kielektroniki (mfumo wa malipo ya kidijitali) kulingana na idadi ya mifugo aliyochanja.
Ruge aliongeza kuwa Halmashauri ya Musoma inakadiriwa kuwa na ng’ombe 118,000, mbuzi 61,852 na kondoo 42,862. Hata hivyo, hadi sasa wamefanikiwa kuchanja ng’ombe 63,700 sawa na asilimia 53, mbuzi 15,529 sawa na asilimia 25, kondoo 7,036 sawa na asilimia 16, na ndege kwa asilimia 70.
Alitaja changamoto kubwa kuwa ni baadhi ya wafugaji kuficha mifugo yao kutokana na imani potofu kwamba chanjo inaweza kuua mifugo, licha ya elimu kutolewa kuhusu umuhimu wa chanjo hizo. Pia, idadi ndogo ya siku zilizopangwa kwa ajili ya chanjo imekuwa changamoto kutokana na ukubwa wa eneo la halmashauri.
Aidha, Ruge aliomba Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi kuwasaidia upatikanaji wa usafiri wa gari kwa ajili ya kufuatilia utekelezaji wa miradi mbalimbali, ikiwemo ya chanjo, katika Halmashauri ya Musoma.






