Na Mwandishi Wetu, Mwanza.
Taasisi isiyo ya kiserikali ya The Desk and Chair Foundation imeonyesha moyo wa huruma na kuguswa na maisha ya kijana aliyejikuta akikwama kielimu kutokana na mazingira magumu ya maisha, kwa kumlipia ada ya mwaka wa kwanza ya masomo chuoni.
Akizungumza na waandishi wa habari William Kabashi kijana aliyekuwa amekata tamaa ya kuendelea na masomo anaeleza kuwa hatua hiyo ni kama ndoto iliyotimia, kwani alipoteza matumaini ya kuendelea na elimu baada ya mama yake mzazi kufariki dunia akiwa bado yupo kidato cha kwanza.
“Baada ya mama kufariki, maisha yangu yalibadilika kabisa. nilibaki peke yangu nikihangaika kutafuta namna ya kuendelea na shule kwa muda wote wa sekondari nilijitafutia vibarua ili niweze kumaliza masomo yangu. nimehitimu kidato cha nne mwaka 2023 kwa daraja la tatu,” anaeleza kijana huyo kwa sauti ya shukrani.
Mwaka 2024, alichaguliwa kujiunga na Chuo cha Utumishi wa Umma Kampasi ya Tabora, lakini hali ngumu ya maisha ilimfanya ashindwe kuendelea na masomo kwa wakati hali hiyo ilimlazimu kutafuta msaada kupitia waandishi wa habari walioguswa na kisa chake na kuamua kumsaidia.
“Namshukuru Mungu kwa kuwa waandishi walikuwa kama mwanga mpya katika maisha yangu. walinitafutia misaada na hatimaye wakaniunganisha na The Desk and Chair Foundation nilijiunga rasmi na chuo mwezi Machi mwaka huu na sasa ninaendelea na masomo kwa bidii kubwa nawaomba Watanzania waendelee kuniunga mkono kwa miaka miwili iliyosalia ili niweze kutimiza ndoto zangu,” aliongeza kwa shukrani.
Kwa sasa, ada na michango yote ya mwaka wa kwanza imelipwa kikamilifu.
Akizungumza mara baada ya kukabidhi rasmi malipo ya ada hiyo, Mwenyekiti wa The Desk and Chair Foundation, Sibtain Meghjee, alisema taasisi hiyo imeguswa na moyo wa juhudi wa kijana huyo pamoja na changamoto alizopitia, hivyo wakaamua kumsaidia kwa moyo wa huruma na upendo.
“Tulipopata taarifa za kijana huyu kupitia kwa waandishi wa habari, tuliguswa sana. Tulishirikiana na wadau wengine na leo tumekamilisha malipo ya ada ya mwaka wa kwanza iliyokuwa imebaki kiasi cha shilingi 370,000 tunampongeza kijana huyu kwa juhudi zake na nia ya dhati ya kuendelea na masomo,” alisema. Meghjee.
Aidha, alitoa shukrani kwa waandishi wa habari kwa mchango wao mkubwa katika kufikisha taarifa hiyo kwao, akisema kuwa ni mfano mzuri wa ushirikiano unaoweza kuleta mabadiliko kwa jamii.
“Waandishi wamefanya kazi kubwa sana. Bila wao, huenda taarifa hii isingetufikia tunaamini kwa kushirikiana kama jamii, tunaweza kuokoa maisha ya vijana wengi wenye ndoto kubwa lakini waliokata tamaa kwa sababu ya ukosefu wa msaada,” aliongeza.
Meghjee alisisitiza kuwa taasisi yake itaendelea kumfuatilia kijana huyo na kutoa ushirikiano katika mwaka wake wa pili na wa mwisho wa masomo, akiwahimiza wale wanaomsimamia kuhakikisha anamaliza vizuri.
“Tunajivunia kumuona kijana huyu akisonga mbele ameonyesha ari ya kujifunza na tunataka awe mfano kwa wengine. Tunaomba taarifa za vijana wengine wenye mahitaji kama haya zifikishwe kwetu, bila kujali dini, rangi au kabila, ili nasi tuweze kuwasaidia.”
Kwa hatua hiyo, kijana huyu sasa anaendelea na masomo yake kwa matumaini mapya, akiamini kuwa safari yake ya elimu itafika mbali kwa msaada wa watu wenye moyo wa huruma na upendo kama walivyoonyesha The Desk and Chair Foundation pamoja na waandishi wa habari.