Na Waf – Dodoma
Tanzania imepiga hatua kubwa katika suala la uzazi wa mpango katika kipindi cha miongo mitatu iliyopita, hatua ambazo zimeendelea kuboresha afya ya jamii na kuchangia maendeleo ya taifa.
Hayo yamebainishwa Septemba 26, 2025, na Mkurugenzi wa Huduma za Uuguzi na Ukunga, Bi. Ziada Sela, akimwakilisha Mganga Mkuu wa Serikali, Dkt. Grace Magembe, wakati wa maadhimisho ya Siku ya Uzazi wa Mpango Duniani yaliyofanyika Jijini Dodoma.
Bi. Sela amesema uzazi wa mpango bado ni kipaumbele cha kitaifa na nyenzo muhimu ya kupunguza umaskini, kupunguza vifo vya akina mama na watoto, pamoja na kuwawezesha wanawake kufanya maamuzi huru na ya kuwajibika kuhusu idadi ya watoto na muda wa kuwapata.
Ameeleza kuwa hali hii itawawezesha wanawake kuendelea na elimu, kufuata ndoto zao za kikazi na kushiriki kikamilifu katika maendeleo ya kiuchumi.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Msaidizi wa Afya ya Uzazi wa Mama na Mtoto, Dkt. Nassoro Mzee, ameipongeza Serikali pamoja na wadau mbalimbali kwa kuchangia fedha ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora za uzazi wa mpango.
“Uzazi wa mpango ni nguzo muhimu na afua bora ya kupanga maisha mazuri. Kama nchi tulianza kushuka katika mwenendo wa matumizi ya huduma za uzazi wa mpango, lakini tunashukuru Serikali kwa kuweka fungu la fedha pamoja na wadau wengine wanaojitolea kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora,” amesema Dkt. Mzee.
Aidha, Msaidizi wa Mwakilishi wa UNFPA Tanzania, Dkt. Majaliwa Marwa, amesema licha ya kuwepo kwa pengo kubwa la rasilimali fedha lililojitokeza hivi karibuni na kuleta changamoto katika utekelezaji wa huduma za uzazi wa mpango, Serikali ya Tanzania kwa kushirikiana na UNFPA, FCDO, Sweden na BMGF imechukua hatua madhubuti kwa kutenga takribani Shilingi Bilioni 23.6 kwa mwaka wa fedha 2024/2025 kwa ajili ya huduma hizo.
Amesisitiza kuwa ni muhimu kubainisha njia mpya za ushirikiano kati ya sekta ya umma na binafsi ili kuwawezesha vijana kutengeneza kesho yao.
Lengo la maadhimisho haya ni kujenga uelewa kwa jamii, wadau mbalimbali na watoa maamuzi kuhusu umuhimu wa uzazi wa mpango kwa afya ya mama na mtoto, pamoja na kuimarisha
Chanzo: wizara ya afya