Na Angela Sebastian- Bukoba
Zaidi ya wahamiaji haramu 800 wamekamatwa katika maeneo mbalimbali ya Mkoa wa Kagera ndani ya mwezi Juni mwaka huu ambapo, baadhi yao tayari wamerudishwa katika nchi zao na wengine wakifuata taratibu za na sheria za nchi zinavyoelekeza.
Akizungumza na waandishi wa habari Kamishna Msaidizi wa Uhamiaji Mkoa wa Kagera Petro Malima amessema wahamiaji hao wengi wao hutokea nchi jirani na huingia kwa njia zisizo rasmi.
Amesema kwa kipindi cha mwezi Juni mwaka huu walikamatwa wahamiaji 725,ambao ni raia wa Burundi ni 514,Uganda 59,Rwanda 41,Kenya mmoja DRC sita,Ethiopia mmoja,China watano,Pakistan mmoja, Watanzania 53 na watu wengine ambao walikuwa wanatafuta urahia ni 44.
"Unaweza kushangaa kwanini Watanzania, ni wale ambao wanapatikana na makosa kama vile wamekutwa na wahamiaji haramu au makosa ya kawaida ambayo yanaangukia kwenye makosa ya uhamiaji"ameeleza Malima
Amesema wahamiaji wapatao 637 waliondolewa kutokana kutokuwa na shaka nao pia kuhusu waethiopia,wachina,Pakistan na Drc hao ni wale ambao wanakuwa hawana vibali ila waliingia kihalali na paspoti zao ni nzuri ila muda wao umeisha wanajisahau hao wanapewa utaratibu mwingine.
Amesema warundi 514, waganda 59 na Wanyarwanda 41 hao walikamatwa kutokana na msako ambapo wamerejeshwa kwao kutokana na mahusiano ya nchi za Afrika Mashariki,pia msako huo ni zoezi endelevu kwa ajili ya kuimalisha usalama wa nchi, maana wakiachwa na kuwa wengi mamlaka zitashindwa kuchukua hatua yoyote hivyo wanaweza kuibua hoja kuwa walizaliwa Tanzania.
Amesema wamegundua sababu zinazowafanya wahamiaji kuja Tanzania kuwa ni pamoja na kutafuta vibarua kwenye mashamba makubwa mfako ya miwa na ya watu binafsi kwenye migomba na kahawa.
Ameongeza kuwa kwa mwezi huu wa saba wahamiaji haramu wengine zaidi ya 100 walikamatwa katika operesheni maalum ya kuondoa wahamiaji haramu ili kuhakikisha usalama wa mipaka ya Tanzania unalindwa ipasavyo.
Kamishna Msaidizi wa Uhamiaji Malima amewataka wananchi wa Mkoa wa Kagera kuendelea kutoa taarifa na ushirikiano kwa vyombo vya usalama ili kuwabaini na kuwachukulia hatua wahamiaji haramu kwasababu watakapo achwa na kubaki katika eneo fulani kwa muda mrefu mwisho watajimilikisha ardhi na kujikuta ndiyo viongozi wa siku za mbeleni.