Na Angela Msimbira, Seoul – Korea
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kupitia Ofisi ya Rais – TAMISEMI, imewasilisha mpango wa upanuzi wa Mfumo wa Kielektroniki wa Taarifa za Afya (GOTHOMIS) katika Mkutano wa Kimataifa wa TEHAMA ya Afya unaofanyika Seoul, Korea Kusini.
Akizungumza kwenye mkutano huo, Mkurugenzi Msaidizi Idara ya TEHAMA Melkiory Baltazary kutoka Ofisi ya Rais -TAMISEMI amesema matumizi ya mfumo huo yamefikia takribani asilimia 83 ya vituo vya kutolea huduma za afya msingi nchini, licha ya changamoto kama uhaba wa wataalamu wa TEHAMA, uelewa kwa watumiaji, na miundombinu hafifu ya umeme na intaneti.
Amesema Tanzania inapendekeza maboresho ya GOTHOMIS ikiwemo mafunzo ya nyongeza kwa watumiaji, kuendelea kuboresha mfumo kuufanya uwe rafiki na rahisi zaidi, matumizi ya teknolojia kama akili bandia (AI) kumsaidia mtoa huduma, na uboreshaji wa miundombinu ya mawasiliano na nishati.
Kwa upande wake, Dkt. Kingho Kim, mtaalamu wa afya ya umma kutoka Korea, ameipongeza Tanzania kwa hatua ilizofikia na kueleza kuwa Korea imefanikiwa kupitia uongozi, uwekezaji wa kimkakati, na ushirikiano wa sekta binafsi na umma katika mifumo ya afya.
> “Mfumo bora wa afya unahitaji sera thabiti, wataalamu, miundombinu na usimamizi wa taarifa kwa wakati,” amesema Dkt. Kim.
Tanzania ilitoa shukrani kwa Serikali ya Korea kupitia KOICA kwa kusaidia awamu ya kwanza ya mradi huo mkoani Dodoma, na kuomba ushirikiano huo kuendelezwa katika awamu ya pili ya utekelezaji kitaifa.