Na Angela Sebastian
Bukoba: Jitihada za Mbunge wa Jimbo la Bukoba Mjini wakili Stephen Byabato zimewezesha miradi minne yenye thamani ya shilingi bilioni 40 ya maendeleo kukabidhiwa kwa wakandarasi ambayo ilikwama kwa muda mrefu kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo za kisiasa.
Miradi hiyo ya ujenzi wa soko kuu la Bukoba,ujenzi wa stendi ya mabasi,kingo za mto Kanoni na upanuzi wa barabara kilometa 10.7 za Minispaa ya Bukoba ambacho kilikuwa ni kilio cha wananchi wa Bukoba cha muda mrefu.
Wakili Byabato ameishukuru Serikali kwa kuridhia kutoa fedha za kutekeleza miradi hiyo iliyokuwa ikisubiriwa kwa hamu kubwa na wakazi wa Manispaa ya Bukoba .
"Mwaka 2020 wakati naomba ridhaa ya kugombea ubunge nilimpelekea hayati mzee John Magufuli aliyekuwa Rais wa hawamu ya tano maombi saba ambapo alirejesha matatu ambayo ni miradi ya soko,kingo za mto Kanoni na standi kuu ambapo aliahidi kuhakikisha miradi hiyo inatekelezwa"ameeleza Byabato
"Wakati napambana kuhangaikiwa utekelezaji wa miradi hiyo kuna baadhi ya watu walikuja kunizuia na kunieleza kuwa nikifuatilia hiyo miradi nitakosa ubunge,nikawajibu soko litajengwa na mimi sio wa kwanza kuwa mbunge hapa wala sitakuwa wa mwisho lazima miradi itekelezwe"ameongeza Mbunge
Anasema sasa yeye hafanyi tena siasa za maneno bali za vitendo na wanaodai kuwa hakushiriki katika miradi hiyo ya maendeleo anawaombea kwa mwenyezi Mungu.
Manispaa ya Bukoba ni miongoni mwa miji 15 ya awamu ya pili zinazotekeleza miradi ya TACTICS, lengo likiwa ni kupendezesha miji na kuongeza mapato ya ndani.
Wakandarasi walioshinda zabuni ya kutekeleza Miradi ya TACTICS Manispaa ya Bukoba yenye thamani ya shilingi bilioni 40 wamekabidhiwa maeneo ya kutekeleza miradi katika Manispaa ya Bukoba mkoani Kagera.
Kwa upande wa mkuu wa Mkoa wa Kagera hajati Fatma Mwassa amesema wakandarasi wamekabidhiwa maeneo ya ujenzi wa Soko Jipya la Manispaa ya Bukoba, Stendi ya Mabasi Kyakailabwa, ujenzi wa kingo za Mto Kanoni zenye urefu wa kilometa 7.3 pamoja na mradi wa ujenzi wa barabara kilometa 10.75 ukiambatana na usimikaji wa taa 423 za barabarani.
Amesema miradi hiyo imegawanywa katika makundi mawili ambapo Mkandarasi mzawa M/s Dimetoclasa Realhope Limited atajenga soko na Stendi ya Mabasi Kyakailabwa kwa gharama ya shilingi bilioni 18.9.
Ameongeza kuwa Mkandarasi wa kigeni M/s Shandon Luqiao Group Company Limited atajenga barabara kilometa 10.75, kingo za Mto Kanoni kilometa 7.3 na kuweka taa za barabarani 423 kwa gharama ya shilingi bilioni 21.3.
Amesema matarajio yake ni kuona miradi hiyo inakamilishwa kwa wakati kulingana na mkataba ambapo wamepewa kipindi cha miezi 15 kuanzia Julai 15, 2025 hadi Oktoba 14, 2026.
Amesema Miradi hiyo inatarajia kuwa kichocheo cha ongezeko la uchumi wa Manispaa ya Bukoba na mkoa wa Kagera kwa ujumla kwa kutengeneza maelfu ya ajira kwa vijana lakini pia kuwa kivutio kwa wakazi wa mkoa huo na wageni kutoka nje.