Kamishna wa Ustawi wa Jamii kutoka
Wizara ya Maendeleo ya Jamii Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Dkt. Nandera
Mhando amewataka wadau wanaotekeleza afua za Watoto kuongeza nguvu na kudhibiti
Watoto wanaoishi na kufanya kazi mtaani.
Dkt. Nandera ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Kitaifa ya Kuratibu Afua za
Watoto wanaoishi na kufanya kazi mtaani
amesema hayo Julai 25, 2025, katika kikao cha tathmini ya utekelezaji wa
majukumu ya kamati hiyo.
Kabla ya kikao hicho, kamati imetembelea dawati la huduma za Ustawi wa Jamii
katika Kituo cha Mabasi cha Magufuli jijini Dar es Salaam kwa lengo
na kutathimini utoaji wa huduma za ustawi kwa watoto.
Dkt. Nandera amesema ni muhimu kwa wadau wote wanaotekeleza Afua za Watoto kuhakikisha
wanatoa huduma stahiki kwa mujibu wa sheria na miongozo iliyopo ili tuweze
kubailiana na changamoto ya Watoto wanaoishi na kufanya kazi mtaan.
Dkt. Nandera amesema miongoni mwa mambo yaliyojadiliwa ni tathmini ya
utekelezaji wa majukumu ya Kamati hiyo na wadau ambao wanahusika katika kuzuia
na kuokoa watoto wanaoishi na kufanya kazi mtaani.
"Kamati imejadili njia za ugemaji fedha kutoka kwa wadau ili kusaidia
kuboresha utoaji wa huduma za ustawi kwa Watoto ikiwemo makao ya Watoto katika
maeneno mbalimbali nchini." amesema Dkt. Nandera
Naye Mjumbe wa Kamati hiyo Mkaguzi wa Polisi Kanda Maalum Dar Es Salaam
Mdathiru Kato Makori amesema Jeshi la Polisi linaendelea na operesheni
mbalimbali katika vituo vya mabasi ili kuwabaini watoto wanaoishi na kufanya
kazi katika maeneo hayo na kuwaokoa kwa kushirikiana na Maafisa Ustawi wa Jamii.
Aidha Mkaguzi wa Polisi Kato ametoa wito kwa jamii kutoa ushirikiano pamoja na
wazazi kutimiza wajibu wa malezi kwa Watoto ili kuzuia wimbo la watoto kuishi
na kufanya kazi mtaani.
Kwa upande wake Afisa Ustawi wa jamii Mkoa wa Dar Es Salaam Nyamara Elisha
amesizitiza wananchi kuripoti matukio yote ya unyanyasaji na utesaji unaofanywa
kwa watoto katika mitaa ili kusaidia vyombo vya sheria kuchukua hatua kwa wote
wanaobainika kufanya vitendo hivyo.