Ripoti ya mwaka 2024 kutoka Mkoa wa Pwani imeonesha ongezeko la vitendo vya ukatili wa kijinsia na kijamii – takriban matukio 7,000 yameripotiwa, ongezeko la 15% ikilinganishwa na mwaka uliopita. katika twakwimu hiyo 60% ya matukio ni ukatili wa kihisia – matusi, vitisho, kejeli na dharau zinazovunja utu hasa wa wanawake na watoto. 30% ni ukatili wa kimwili – vipigo, kuchomwa moto, na madhara ya moja kwa moja kwa mwili. 10% ni ukatili wa kingono – ikijumuisha ubakaji, ulawiti, na unyanyasaji wa kingono kwa mabinti, wanawake na hata watoto wa kiume.
Takwimu hizi zinatoa picha halisi ya hali ya kushtua inayohitaji hatua za haraka na za pamoja kutoka kwa jamii, serikali na wadau wa haki za binadamu.
Katika kukabiliana na changamoto hii, Shirika la CYDAD (Centre for Children, Young People and Adult Development), likiwa mwanachama wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC), limechukua hatua mbalimbali kukabiliana na ukatili wa kijinsia kwa kutoa elimu ya kijinsia na mbinu za kujikinga na ukatili kwa wanawake, mabinti na watoto kupitia kampeni na warsha; kuhamasisha ushiriki wa wanaume na wavulana katika mapambano dhidi ya ukatili; kuendesha mafunzo ya ujasiriamali na kuweka akiba kwa wanawake na mabinti ili kuwawezesha kiuchumi na kupunguza utegemezi unaochangia ukatili; pamoja na kuwezesha huduma za ushauri nasaha na msaada wa kisheria kwa waathirika, huku wakihakikisha haki inatendeka kwa kufuatilia mashauri hadi mwisho.
Kupitia mshikamano, elimu, na uwezeshaji, tunaweza kujenga jamii isiyovumilia ukatili wa aina yoyote. Sauti yako ina nguvu. Tuchukue hatua sasa.
Chanzo: THRDC
#UsalamaWaWanawake #HakiZaBinadamu #PingaUkatili #CYDAD #THRDC #MkoaWaPwani #UwezeshajiWanawake #Tanzania #SemaUsikike #StopGBV