Naibu Waziri Nishati, Mhe. Judith Kapinga amesema Serikali kupitia Wizara ya Nishati imetumia takribani shilingi bilioni 107.36 kupeleka umeme kwenye Vijiji vyote474 vya Mkoa wa Simiyu.
Kapinga ameyasema hayo
leo Juni 18, 2025 wakati akitoa tathmini ya hali ya upatikanaji wa umeme Mkoa
wa Simiyu na maendeleo ya usambazaji wa nishati safi ya kupikia wakati wa
kuhitimisha ziaraya kikazi ya Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan katika Mkoa wa
Simiyu.
"Mheshimiwa Rais
baada ya kumaliza upelekaji wa umeme kwenye Vijiji, hivi sasa tunapeleka umeme
kwenye Vitongoji na hivi sasa tunatekeleza miradi ya umeme kwenye Vitongoji 638
kati ya Vitongoji 1,408 vya Mkoa wa Simiyu”. Amesema Mhe. Kapinga
Ameongeza kuwa Serikali
itajenga kituo cha kupokea na kupoza umeme cha Simiyu kupitia mradi wa gridi
imara na kuongeza kuwa hivi sasa Mkoa wa Simiyu unapata huduma ya umeme kutoka
Mikoa mitatu ya Shinyanga, Mwanza na Mara.
Amesema kituo hicho
kitazidi kuimarisha hali ya umeme Simiyu na hivyo kuwa muhimu kwa maendeleo ya
watu wa Simiyu.
Amesema mradi wa gridi
imaramkoani Simiyu una sehemu mbili ambazo ni ujenzi wa njia ya kusafirisha
umeme kutoka Ibadakuli Shinyanga hadi Bariadi utakaojengwa kwa takribani
shilingi bilioni 48 na ujenzi wa kituo cha kupokea na kupoza umeme cha Bariadi
kitakachojengwa kwa gharama ya shilingi bilioni 49.
Ameongeza kuwa,
kukamilika kwa mradi wa kituo cha kupokea na kupoza umeme Mkoa wa Simiyu
utawezesha Mkoa kuwa nauwezo wa megawati 150.
Kuhusu Nishati Safi ya
Kupikia, Kapinga amesema Mkoa wa Simiyu umepata mitungi ya gesi yaruzuku
takribani 16,275 ambayo yote tayari imeshachukuliwa na wananchi kwa bei ya
ruzuku.