Na Ghati Msamba-Dar es Salaam.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Kazi, Ajira, Vijana na Watu Wenye Ulemavu, Mhe. Ridhiwani Kikwete, amefungua rasmi Mkutano Mkuu wa Mwaka wa Chama Cha Waajiri Tanzania (ATE) uliofanyika jijini Dar es Salaam tarehe 18 Juni 2025.
Mkutano huo, ambao umehudhuriwa na wadau mbalimbali wa sekta ya ajira, ulitanguliwa na uwasilishaji wa taarifa za kiutendaji za mwaka na kongamano lililojadili mabadiliko ya sheria za kazi pamoja na athari zake kwa waajiri na waajiriwa katika kuimarisha tija mahala pa kazi.
Akizungumza katika mkutano huo, Mhe. Kikwete alieleza kuwa serikali inatambua na kuthamini mchango wa wadau wote wakuu katika Utatu wa mashirikiano baina ya Serikali, Waajiri na Wafanyakazi. Alibainisha kuwa mabadiliko ya sheria za kazi yanalenga kuboresha mazingira ya kazi na kuhakikisha haki na wajibu vinazingatiwa kwa pande zote.
“Ninawapongeza sana ATE kwa ushirikiano wao mkubwa katika mchakato wa mabadiliko ya sheria hizi na kwa kushiriki kikamilifu katika kuhakikisha tunakuwa na sheria bora za kazi zinazozingatia matakwa ya ndani na viwango vya kimataifa,” alisema Mhe. Kikwete.
Aidha, Waziri aliwashukuru wadau wa maendeleo, hususan Shirika la Kazi Duniani (ILO), kwa kuendelea kushirikiana na Tanzania katika masuala ya ajira na kazi. Alitumia nafasi hiyo pia kuwasilisha salamu za pongezi kutoka kwa Mkurugenzi Mtendaji wa ILO, Cde. Gilbert F. Houngbo, kwa ATE na wadau wote waliofanikisha mkutano huo muhimu.
Mkutano huo umetajwa kuwa wa mafanikio makubwa kwa kutoa majukwaa ya kujadili changamoto, mafanikio na njia bora za kushirikiana kwa lengo la kuboresha mazingira ya kazi nchini.