Waziri Mavunde Ampongeza Mkuu wa Mkoa wa Mara Kwa Kuandaa Kongamano la Madini

0


Na Ghati Msamba-Musoma

Waziri wa Madini, Anthony Mavunde, amempongeza Mkuu wa Mkoa wa Mara, Kanali Evans Mtambi, kwa kuandaa kongamano la maonyesho ya madini litakalowakutanisha wadau mbalimbali wa sekta hiyo ili kujifunza mbinu bora na matumizi ya teknolojia ya kisasa katika uchimbaji wa madini.

Akizungumza wakati wa hafla ya uzinduzi wa kongamano hilo, Waziri Mavunde alisema kuwa Mkoa wa Mara ni miongoni mwa mikoa iliyofanya vizuri katika sekta ya madini, ambapo unachangia asilimia 18 ya mapato ya madini kitaifa. Alisisitiza kuwa sekta hiyo ina mchango mkubwa katika maendeleo ya kiuchumi ya mkoa huo na Taifa kwa ujumla.

"Sekta ya madini ndiyo sekta inayoongoza kwa ukuaji wa kasi na inakwenda kuleta mageuzi makubwa ya kiuchumi nchini," alisema Waziri Mavunde.

Akiyataja mafanikio yaliyopatikana katika kipindi cha miaka minne chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan, Waziri Mavunde alisema kuwa sekta ya madini imepata mafanikio makubwa ikiwa ni pamoja na kupokea shilingi bilioni 224 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo.

Fedha hizo zimetumika kujenga maabara za kupima sampuli za madini katika mikoa ya Dodoma, Geita na Chunya ili kupunguza gharama kwa wachimbaji. Aidha, amesema wizara imenunua helikopta yenye uwezo wa kuchimba chini ya ardhi ili kurahisisha shughuli za utafiti wa madini.

Katika mwaka wa fedha 2022/23, sekta ya madini iliagizwa kuchangia asilimia 10.1 ya mapato ya Taifa. Mwaka huu wa fedha 2024/25, mchango wa sekta hiyo umeongezeka hadi kufikia shilingi bilioni 753 ikilinganishwa na bilioni 1.162 mwaka 2015. Kati ya mapato hayo, asilimia 40 yametokana na wachimbaji wadogo kufuatia marekebisho ya sheria yaliyoruhusu ushiriki wao mkubwa zaidi katika sekta hiyo.

Aidha, Waziri Mavunde alieleza kuwa kwa mwaka huu, wizara yake imekusudia kukusanya kiasi cha shilingi trilioni 1 ambapo tayari sehemu kubwa ya fedha hizo zimeanza kuingizwa serikalini.

"Ni marufuku kwa mtu yeyote kumuingiza mchimbaji mdogo katika leseni yake. Badala yake, fanyeni mikataba rasmi na wahakikishe mnawalipa wenye maeneo ya uchimbaji pindi mtakapopata wawekezaji, ili kuepusha migogoro," alionya Waziri Mavunde.

Aliongeza kuwa Wizara ya Madini imepanga kufanya utafiti wa kina kuhusu rasilimali za madini ifikapo mwaka 2030 ili kuhakikisha matumizi endelevu na ya tija kwa taifa.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Madini la Taifa (STAMICO), Nchagwa Marwa, alimshukuru Rais Samia kwa kuweka mazingira rafiki kwa wachimbaji wadogo na wakubwa, hali iliyoleta ufanisi na kuongeza uzalishaji katika sekta hiyo.

Naye Mwenyekiti wa Chama cha Wachimbaji wa Madini Mkoa wa Mara (MAREMA), David Peter, alisema kuwa kongamano hilo litakuwa chachu ya mageuzi chanya kwa wachimbaji wa madini, kwani litawezesha kutatua changamoto zao na kuboresha utendaji kazi wao.

Aidha, alimpongeza Rais wa wachimbaji wa madini kitaifa kwa juhudi kubwa alizofanya kuhakikisha kuwa wachimbaji wadogo wanawezeshwa kushiriki kikamilifu katika uchumi wa madini.

Afisa Madini wa Mkoa wa Mara, Amin Msuya, akiwasilisha taarifa ya mafanikio ya sekta ya madini kwa kipindi cha 2021–2025, alisema uchimbaji umeongezeka kwa kiasi kikubwa na kwamba mkoa huo una uwezo wa kufikia malengo ya ukusanyaji wa mapato ya shilingi milioni 210 kwa mwaka wa fedha 2025.

Katika hotuba yake, Rais wa  shirikisho la vyama Vya wachimbaji wa madini John  Binna alimpongeza  Rais Samia kuwa ni kiongozi msikivu. Alitoa wito kwa wachimbaji kumtumia Waziri wa Madini kama kiungo muhimu katika kuhakikisha kuwa wanapata haki na manufaa ya shughuli zao kwa kufuata sheria za umiliki wa leseni.

Binna amewataka wachimbaji wadogo kuhakikisha wanabiresha shughuli zao Ili kumiliki uchumi kupitia sekta za madini Kwa kuwa changamoto nyingi zilizokuwa zikiwakabili hapo awali zimetatuliwa na serikali.  Na kuwataka kubadili fikira zao za kufikiri namba ya kuhama kutoka wachimbaji wadogo na kuwa wa kati na wakubwa Kwa kuwa mazingira ya kazi yao yameboreshwa Kwa kiasi kikubwa.

Mkuu wa Mkoa wa Mara, Kanali Evans Mtambi, alihitimisha kwa kusisitiza kuwa Mara ni mkoa wa pili kitaifa kwa ukusanyaji wa mapato yatokanayo na madini, hivyo wachimbaji wadogo wanapaswa kupewa elimu na mafunzo ili kuongeza tija na ufanisi katika shughuli zao.






Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.
Post a Comment (0)

#buttons=(Accept !) #days=(20)

Our website uses cookies to enhance your experience. Learn More
Accept !
To Top