đŸ‘‰Lengo ni kuondokana na migogoro sehemu za uchimbaji.
Naibu waziri wa Madini Dkt. Steven Kiruswa amewataka wachimbajibwadogo wa madini kuijua Sheria ya Madini Sura 123 na Kanuni zake ili kuondokana na migogoro sehemu za uchimbaji madini ambayo hupelekea kurudisha nyuma maendeleo ya kazi.
Dkt.Kiruswa ameyasema hayo Juni 22, 2025 Wilaya ya Ikungi wakati wa ziara yake ya kukagua shughuli za uchimbaji na ushalishaji madini pamoja na kusikiliza migogoro iliyopo katika machimbo mbalimbali katika kata ya Matongo na Mang'onyi mkoani Singida.
Dkt.Kiruswa ameeleza kuwa kutokana na utafiti uliofanyika imeibainika kuwa, moja ya sababu inayoleta migogoro katika maeneo ya uchimbaji ni pamoja na kufanya uchimbaji pamoja na kumiliki leseni ya uchimbaji bila kuijua Sheria ya Madini na Kanuni zake ambapo amewataka wataalam kutoka Ofisi ya Madini Mkazi Singida kutoa elimu kuhusu Sheria ya Madini na Kanuni zake.
Dkt. Kiruswa ameongeza kuwa, pamoja na Sheria ya Madini pia wachimbaji wadogo wanatakiwa kufahamu kuhusu Mpango wa Ushirikishaji Jamii zinazozunguka mgodi (CSR) na Mpango wa Manunuzi kwa Wazawa (Local Content) kwa faida ya wamiliki wa leseni kujua sehemu ya wajibu wao.
Akielezea kuhusu changamoto zilizopo kwa wachimbaji wadogo wa Kata Matongo , Dkt. Kiruswa ameeleza kuwa, Serikali inatambua changamoto mbalimbali zilizopo akitolea mfanyakazi changamoto ya Barabara , Nishati ya Umeme na Maji na kuahidi kuwa katika Mwaka wa Fedha 2025/2026 zitapewa kipaumbele kuzitatua
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Ikungi , Thomas Apson amesema, wilaya ya Ikungi imefanikiwa kupunguza migogoro katika maeneo mbalimbali ya wachimbaji wadogo ambayo ilikuwa inahusisha ardhi , leseni na maduara ya uchimbaji katika Kata zinazoizunguka wilaya ya Ikungi.
Akibainisha kuhusu mchango wa Sekta ya Madini, Apson ameipongeza Wizara ya Madini kwa juhudi inazofanya katika mageuzi ya mifumo ya kiutendaji na ushirikishaji wa kisekta ambayo inaleta matokeo chanya kiuchumi.