Naibu Katibu Mkuu-Elimu, Ofisi ya Rais TAMISEMI Mhe. Atupele Mwambene amewasisitiza Viongozi wa elimu Sekondari na msingi kufanya kazi kwa ushirikiano na kwa upendo ikiwa lengo ni kuboresha sekta ya elimu nchini.
Wito huo ameutoa leo Juni 20, 2025 wakati wa kufunga kikao kazi cha Tathmini ya Utekelezaji wa Shughuli za Elimu kwa kipindi cha Januari hadi Juni 2025, kilichowakutanisha Maafisa Elimu wa Mikoa na Halmashauri katika viwanja vya Kichangani, Mkoani Iringa.
"Tunajukumu la kuimarisha ushirikiano baina yetu kwa maana sisi kama Ofisi ya Rais - TAMISEMI na Ofisi za Mikoa, Halmashauri na Shule lakini vilevile niwaombe sana Viongozi muwajali Watumishi" amesema Mwambene
Vilevile amesisitiza kuhusu uboreshaji wa miundombinu ya shule kuimarisha mazingira ya kufundishia na kujifunzia jambo ambalo litapelekea kuongeza viwango vya ufaulu nchini.
"Tunajukumu la kusimamia kwa ukamilifu ufundishaji na na ujifunzaji shuleni kwa lengo la kuboresha elimu nchini" amesisitiza
Aidha amesisitiza kuwa matumizi ya mfumo ulioboreshwa wa ukusanyaji wa takwimu ikisimamiwa ipasavyo kutapunguza kwa kiasi kikubwa usumbufu uliopo kuombana takwimu mara kwa mara lakini itawezesha kuwa na mipango thabiti.
Kikao kazi hicho ni sehemu ya mikakati ya Serikali kupitia Ofisi ya Rais- TAMISEMI katika kuhakikisha kuwa elimu bora inapatikana kwa kila mtoto wa kitanzania kupitia usimamizi thabiti na ufuatiliaji wa karibu wa utekelezaji wa sera na mipango ya elimu nchini.