Tanzania imepata ushindi wa medali 4 za Shaba kwenye mashindano ya Hisabati Afrika ya Pan African Mathematics Olympiad (PAMO 2025), yaliyofanyika katika Chuo Kikuu cha Botswana jijini Gaborone, kuanzia tarehe 8 hadi 18 Juni, 2025. Medali 3 kati ya hizo ni za washindi watatu wa kundi la jumla, na medali 1 ni kutoka kwenye kundi la wasichana.
Ushindi huo umeiwezesha Tanzania kushika nafasi ya 10 kati ya nchi 23 Barani Afrika, zilizoshiriki mashindano hayo mwaka huu, kwa kupata alama 47 ilikinganishwa na mwaka 2024 ambapo Tanzania ilipata alama 37 na kushika nafasi ya 15 miongoni mwa nchi 25.
Wanafunzi walioshiriki kwenye mashindano hayo ni Rachel Lazaro Nyhasi kutoka shule ya Sekondari Benjamin Mkapa, Elia Enock Deus wa Kibaha sekondari, Numan Benhajj Masoud wa Shamsiye Boys sekondari, Stanley Francis Thomas wa Chang’ombe Sekondari, Shufaa Awadh Mwanga wa Fedha Girls Girls na Stella Ludani Maliti wa Marian Mater-Dei Girls.
Mwaka jana Wanafunzi watanzania walipata medali Nne za shaba (Bronze Medals) kwenye mashindano ya Hisabati Afrika ya Pan African Mathematics Olympiads (PAMO 2024), yaliyofanyika katika chuo kikuu cha Witwatersrand, jijini Johannesburg, Afrika Kusini
Wanafunzi hawa waliodhaminiwa na TCRA kushiriki katika mashindano, wamechangia Tanzania kuendelea kung’ara na kutambulika kimataifa kwenye ufanisi wa taaluma ya somo la Hisabati. Matokeo haya mazuri ni fursa kwa nchi yetu kuwa sehemu ya maendeleo ya Dunia katika nyanja za Sayansi, Teknolojia, Uhandisi na Hisabati (STEM), pamoja nakushiriki kikamilifu na kunufaika na uchumi wa kidijiti unaotegemea TEHAMA.
Chanzo:TCRA