Na Ghati Msamba.
Katika juhudi za kuendeleza na kuimarisha uhusiano wa muda mrefu kati ya Tanzania na Jamhuri ya Watu wa China, mazungumzo ya kihistoria yamefanyika jijini Dodoma kati ya ujumbe wa Ubalozi wa China ukiongozwa na Balozi wa China nchini, Mheshimiwa Chen Mingjian, na mwenyeji wake Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais - Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Ridhiwani Kikwete.
Katika kikao hicho, kilichofanyika Jana jijini Dodoma ,Balozi Chen Mingjian alitumia fursa hiyo ya kujitambulisha rasmi na kueleza dhamira ya nchi yake kuendeleza ushirikiano wa muda mrefu na Tanzania, kwa kuzingatia maeneo muhimu ya maendeleo, hususan katika sekta ya elimu ya ufundi, mafunzo ya ujuzi, na maandalizi ya vijana kukabiliana na changamoto na fursa za mapinduzi ya teknolojia ya kisasa duniani.
Balozi Chen alisisitiza kuwa China itaendelea kushirikiana kwa karibu na Tanzania katika kuwajengea vijana uwezo wa kisasa kupitia mafunzo, programu maalum, na miradi ya pamoja inayolenga kuboresha ajira na ujasiriamali kwa vijana wa Kitanzania.
Kwa upande wa Tanzania, mwenyeji wa kikao hicho Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais - Kazi, Vijana na wenye ulemavu Ridhiwani Kikwete alithibitisha kuwa serikali itaendelea kuenzi na kudumisha uhusiano wa kihistoria kati ya nchi hizi mbili.
Aidha, alieleza kuwa Tanzania iko tayari kuimarisha maeneo yote ya mashirikiano yanayowanufaisha wananchi, hususan katika kukuza ujuzi wa vijana ambao ni nguvu kazi ya taifa.
"Serikali ya Tanzania inatambua na kuthamini mchango mkubwa wa serikali ya China, hususan katika kusaidia mabadiliko makubwa yanayolenga kukuza ujuzi kwa vijana wetu," alisemaw Waziri Kikwete.
"Tunafurahia kuona dhamira yao ya kuandaa maonyesho makubwa ya kazi yatakayowapa vijana fursa za kujiajiri na hata kuajiriwa na makampuni makubwa, yakiwemo ya Kichina hapa nchini."
Kikao hicho kimetajwa kuwa hatua muhimu kuelekea kuimarisha ushirikiano kati ya mataifa haya mawili, na ni uthibitisho wa dhamira ya pamoja ya China na Tanzania kuhakikisha maendeleo jumuishi na endelevu, hasa kwa kizazi kijacho.