Na Aisha Swahib, WAF – Dar es Salaam
Serikali kupitia Wizara ya Afya imepiga hatua kubwa katika kupunguza vifo vya watoto wenye umri chini ya miaka mitano kutoka vifo 67 kwa kila vizazi hai 1,000 mwaka 2016 hadi kufikia vifo 43 kwa kila vizazi hai 1,000 mwaka 2022.
Hayo yamesemwa na Mkurugenzi wa Idara ya Huduma za Afya ya Uzazi, Mama na Mtoto, Dkt. Ahmad Makuwani, leo Machi 4, 2026, wakati akifungua kikao kazi cha kujadili tathmini ya utekelezaji wa mpango mkakati wa Afya ya Uzazi, Mama na Mtoto (RMNCAH + N – One Plan III) jijini Dar es Salaam.
Dkt. Makuwani amesema Tanzania imepata mafanikio makubwa katika kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi kutoka vifo 556 kwa kila vizazi hai 100,000 hadi kufikia vifo 104 kwa kila vizazi hai 100,000, hatua iliyoifanya nchi kutambulika kimataifa kama kinara wa kupunguza vifo hivyo.
Ameeleza kuwa mafanikio hayo yameiwezesha Tanzania kutambulika kimataifa, ikiwemo kumtambua Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan kama kiongozi kinara wa uimarishaji wa huduma za afya ya uzazi, mama na mtoto barani Afrika, pamoja na kutunukiwa tuzo ya kimataifa ya Goalkeepers Award.
Dkt. Makuwani amesema pamoja na mafanikio hayo, bado kuna wajibu wa kushirikisha mataifa mengine hususan barani Afrika kuhusu mikakati iliyowezesha Tanzania kufikia hatua hiyo ili yaweze kujifunza na kupunguza zaidi vifo vya uzazi na watoto chini ya miaka mitano.
Aidha, ameongeza kuwa eneo la kupunguza vifo vya watoto wachanga wenye umri chini ya siku 28 bado linahitaji nguvu zaidi, hivyo kupitia tathmini hiyo, mikakati madhubuti itawekwa ili kupunguza kwa kiwango kikubwa vifo hivyo.
✍️wizara ya afya











